BBI ndiyo dawa ya maridhiano, asema Waiguru
Na CHARLES WASONGA
Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru na aliyekuwa Msimamizi wa Ikulu Matere Keriri wamewataka wanasiasa kuunga mkono ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) wakisema litaleta amani ya kudumu.
Wawili hao walisema Wakenya wote wanaopenda amani wanapaswa kufurahia uthabiti wa kitaifa ambao umeletwa nchini kutokana na muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Walitaka wale ambao wanaanzisha michakato mingine kusitisha mipango hiyo na waunge mkono BBI inayolenga kuleta amani na maridhiano ya kudumu.
Waiguru alipuuzilia mbali mchakato wa mageuzi ya Katiba ya Punguza Mizigo wa wakili Ekuru Aukot akisema haungeweza kufaulu tangu mwanzo.
Gavana huyo alidai kuwa Bw Aukot alikosa kufanya mashauriano na Wakenya ambao ndio wangefaidi kwayo.
“Hii ina maana kuwa mchakato wa Aukot wa Punguza Mizigo ulilenga kutimiza maslahi yake au ya watu fulani ambao wanajitakia makuu. Kwa hivyo, mpango wowote nje ya BBI hauendelezi masilahi ya Wakenya,” akasema Ijumaa alipowahutubia wanahabari nje ya afisi yake mjini Kutus.
Bw Keriri alisema Bw Odinga ataenziwa na vizazi vijavyo kutokana na uamuzi wake wa kukubali kuridhiana kisiasa na Rais Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.
“Baada ya ubishi uliotokana na matokeo ya kura ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2017, taifa liligawanyika kuwili; wafuasi wa Raila kwa upande mmoja na wale wa Rais Kenyatta katika upande mwingine,” Bw Keriri akasema.
Akaongeza: “Kuthibitisha kuwa ana ufuasi mkubwa, Raila aliamua kujiapisha kama rais wa watu. Lakini kupitia uongozi wa busara wa Rais Kenyatta alikomesha umwagikaji wa damu kwa kuondoa maafisa wa polisi kutoka bustani ya Uhuru ambako sherehe hiyo isiyo halali ilifanyika.”
Bw Keriri alisema hata baada ya mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wafuasi wake, Bw Odinga aliweza kuwadhibiti na mkutano ukaisha salama bila watu kuharibu mali.
“Hiki ni kielelezo cha kiongozi mpenda nchi na njia ya kipekee ambayo tunaweza kumshukuru ni kwa kuunga mkono mapendekezo ya BBI. Utekelezaji wa mapendekezo hayo utawezesha taifa hili kuendelea kufurahia amani na uthabiti hata baada ya uchaguzi mkuu wa 2022,” alieleza.
Bw Keriri pia alimshukuru Bw Odinga kwa kukubali kugawana mamlaka na Rais mstaafu Mwai Kibaki baada ya upatanishi ulioongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan kufuatia ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
“Ugavi wa mamlaka na sasa handisheki ni mambo mawili ya kihistoria ambayo Raila atakumbukwa kwayo,” akasema msimamizi huyo wa zamani wa Ikulu wakati wa utawala wa Kibaki.