Bei jumla ya maski yapanda – wafanyabiashra
Na SAMMY WAWERU
BEI jumla ya maski imeanza kupanda huku visa vya maambukizi ya Covid-19 vikionekana kuanza kuongezeka.
Septemba 2020 hadi mapema mwezi huu wa Oktoba, idadi ya maambukizi ya corona iliashiria kupungua ikilinganishwa na miezi iliyotangulia baada ya Kenya kuandikisha kisa cha kwanza Machi 2020.
Kulingana na wafanyabiashara wa maduka ya beijumla jijini Nairobi tuliozungumza nao, wanasema kwa chini ya muda wa juma moja lililopita wameshuhudia kuongeza kwa bei ya maski.
Maski pia barakoa ni baadhi ya vifaa vinavyopendekezwa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani kuvaliwa kufunika mdomo na pua ili kusaidia kuzuia kuambukizwa Covid-19.
“Maambukizi ya corona yalipoanza kupanda tena, nayo bei ya maski ikaongezwa na wanaotuuzia,” mfanyabiashara aliyejitambulisha kama Wanjiku akaambia Taifa Leo.
Mfanyabiashara huyo ni kati ya wauzaji wa bidhaa katika maduka ya beijumla Ukwala Lane, jijini Nairobi.
Akitumia mfano wa maski za bei nafuu zilizoidhinishwa na idara ya afya, alisema katoni ya barakoa 50 awali walikuwa wakiuzia wafanyabiashara rejareja beijumla Sh190.
“Wiki iliyopita, ilipanda tukawa tunawauzia Sh200 kila katoni. Juma hili bei imekwea hadi Sh250,” akadokeza, akionya huenda bei ikapanda hadi mara dufu.
Wafanyabiashara rejareja huuza maski moja Sh20, ingawa kuna zingine za Sh30.
Kauli ya Wanjiku inawiana na ya maduka kadhaa jijini Nairobi tuliyozuru, tukiwa na lengo kubaini kuongezeka kwa bei ya vifaa hivyo muhimu.
“Tunakonunua nasi pia tumeongezewa bei, hivyo basi tunagawana gharama na wafanyabiashara rejareja ili sote tupate faida,” akasema mfanyabiashara mwingine wa beijumla jijini.
Awali, serikali ilikuwa imeonya wanaoongeza kiholela bei ya maski, ikisema inaendelea kuimarisha na kupiga jeki viwanda vinavyotengeneza vifaa hivyo.
Miezi ya kwanza Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa corona, maski za hospitali zilikuwa zinagharimu Sh200.
Zinazoundwa kwa vitambaa zilikuwa Sh50 kila maski, na serikali ilipoweka mikakati kuhakikisha kuna maski za kutosha nchini zilishuka hadi Sh30, Sh20 na zingine Sh10.