Benki 5 zaungana kuzifaa biashara ndogo kwa mikopo bila wadhamini
Na BERNARDINE MUTANU
Benki tano zimeungana kwa lengo la kutoa mikopo kwa wenye biashara ndogo na za wastani.
Wafanyibiashara hao watakuwa na uwezo wa kupata mikopo bila wadhamini. Watakuwa na uwezo wa kupata mikopo kati ya Sh30, 000 na Sh250, 000 kutoka kwa mpango huo unaofahamika kama ‘Stawi’ kupitia kwa simu zao mikononi.
Mkopo huo utalipwa katika muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi 12 na utatozwa riba ya asilimia tisa kwa mwaka.
Ada zingine zitakazotozwa baada ya kutolewa kwa pesa hizo ni asilimia nne za benki, asilimia 0.7 za bima na ushuru wa asilimia 20 za mpango huo.
Mpango huo utasimamiwa na Benki ya Commercial (CBA) Cooperative Bank of Kenya (Co-op Bank), Diamond Trust Bank Kenya (DTB), KCB Bank Kenya na Benki ya NIC.
Wakopaji wazuri watatuzwa kwa kupewa pesa kuambatana na jinsi walivyokopa na kulipa.
“Biashara ndogo na zile za wastani ni muhimu zaidi katika uchumi, lakini biashara nyingi hutatizika kupata ufadhili kuendelea na operesheni zake katika mandhari mabaya ya uchumi,” alisema gavana wa Benki Kuu Patrick Njoroge wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika Soko la Gikomba, Jumatatu.
“Tunafurahia kufanya kazi na benki hizo tano kupunguza ungumu wa kubuni na kukuza mipango mipya ya mikopo kwani zitafanya rahisi kwa wafanyibiashara katika sekta hiyo kupata mtaji,” aliongeza.
Mpango huo ni kati ya juhudi za CBK za kuimarisha viwango vya utoaji wa mikopo.