Habari Mseto

Benki ya NIC itainyanyua Uchumi?

April 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Duka la Uchumi limegeukia Benki ya NIC kulisaidia kukabiliana na changamoto za kifedha linaloshuhudia.

Hii ni kwa mujibu ripoti ya kila mwaka ya duka hilo, huku duka hilo likizidi kukabiliwa na changamoto ya deni kubwa.

Lakini litaanza kushirikiana na benki hiyo baada ya kupata mwekezaji. Kulingana na Mkurugenzi Mkuu Mohamed Mohamed, kazi ya NIC itakuwa ni kuwasaidia watoaji wa bidhaa ambao wanahitaji kubadilisha deni lao katika duka hilo kuwa mtaji.

Mwekezaji anayetarajiwa kuokoa Uchumi anatarajiwa kuipa Sh3.5 bilioni kama mtaji ingawa mwekezaji huyo hajatambulishwa.

Pia duka hilo linatarajia kupata mikopo kutoka kwa serikali na kubadilisha deni pamoja na kuuza kipande cha ardhi Kasarani ili liweze kupata Sh2.6 bilioni.

Uchumi inatarajia kupokea Sh600 milioni kutoka kwa serikali katika awamu ya mwisho ya mkopo wa Sh1.8 bilioni lililopewa na serikali mwanzoni mwa mwaka 2017.