• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Beyond Zero yasifiwa kimataifa

Beyond Zero yasifiwa kimataifa

PSCU na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi (UNAIDS), Gunilla Carlsson ameusifu mpango wa Beyond Zero hasa mchango wake bunifu wa kushughulikia tatizo la maradhi ya ukimwi sawa na utoaji huduma za afya nchini Kenya.

Bi Carlsson alimhakikishia Mama Taifa Bi Margaret Kenyatta kwamba UNAIDS imejitolea kuendelea kuunga mkono harakati zake za kukabiliana na maradhi ya ukimwi na hatua za kusambaza huduma za afya karibu na wananchi kupitia harakati mpya za kushirikisha wahudumu wa afya katika ziara za kutoa huduma hizo nchini Kenya, almaarufu Medical Safaris.

“Wewe ni mtetezi wa kipekee wa afya ya akina mama wajawazito na watoto wachanga. Tunaridhishwa na mchango wako katika sekta ya afya kupitia harakati za shirika la Beyond Zero,” Bi Carlssom akamwambia Bi Kenyatta.

Mkurugenzi huyo alisema hayo Jumanne alipomkaribisha Mama Taifa Margaret Kenyatta katika makao makuu ya shirika la UNAIDS jijini Geneva, Uswizi ambapo Mkewe Rais aliangazia kazi anayofanya kupitia mpango wa Beyond Zero nchini Kenya.

Alitoa wito kwa mashirika husika kuunga mkono utoaji wa huduma za afya nchini Kenya katika kikao hicho kilichohudhuriwa na mamia ya washikadau wa afya jijini Geneva.

Akihutubia kikao hicho, Bi Kenyatta alisema kupitia mpango wa Beyondo Zero alilenga kufanya kitendo cha kipekee ambacho kingewafanya watu wote kuwa makini kushughulikia kuenea kwa maradhi ya ukimwi nchini Kenya kando na kushughulikia afya ya akina na watoto.

“Nilihitaji kuhimiza Serikali, waratibu maongozi wa kitaifa na wa kimataifa kuchukua hatua zaidi kulinda haki za wanawake, kina mama na watoto katika nyanja ya afya.

” Hatua hii ilisaidia kuanzisha harakati za Beyond Zero ambazo zilimulika zaidi utoaji wa huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto,”akasema Bi Kenyatta.

Alisema mpango wa Beyond Zero kupitia Mfumo wa Mkakati wake wa pili wa kutoa huduma wa kipindi cha mwaka wa 2018 hadi 2022, unawekeza katika hatua za kuzuia maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi na kuondoa kabisa hali ya akina mama kusambaza maradhi yao kwa watoto wao wakiwa wanazaliwa, hali ambayo alisema inatishia kuvuruga manufaa yaliyoafikiwa katika kukomesha maambukizi mapya ya ukimwi nchini Kenya.

Mama Taifa alitaja harakati za Medicals Safaris za shirika la Beyond Zero ambao ni mfumo wa kutoa huduma za afya bila malipo karibu na jamii zinazokabiliwa na hatari kwenye maeneo yasiyofikika kwa urahisi nchini, kuwa mfano wa mikakati bunifu ya shirika la Beyond Zero katika kukabili maradhi ya HIV pamoja na changamoto zingine za afya.

Wengine waliozungumza ni Waziri wa Afya Sicily Kariuki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Janga la Ukimwi Dkt Nduku Kilonzo na DKt Cleopa Mailu ambaye ni Balozi wa Kenya nchini Uswizi na Mwakilishi wa Kudumu katika Afisi ya Umoja wa Mataifa Jijini Geneva.

You can share this post!

IEBC yatangaza upya nafasi ya Chiloba baada ya watu...

Wachezaji watishia kugura Chelsea Sarri asipotimuliwa

adminleo