• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Bidco Africa, Thiwasco wazindua vituo 100 vya usafi wa mikono

Bidco Africa, Thiwasco wazindua vituo 100 vya usafi wa mikono

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya BIDCO Africa Ltd na ile ya maji ya Thiwasco Water Company Ltd pamoja na washika dau wengine wamezindua maeneo 100 yatakayotumika na wananchi na wakazi wengine kusafisha mikono.

Mkurugenzi wa Thiwasco Water Company Ltd Bw Moses Kinya alisema ni muhimu kwa ushirikiano huo kwa minajili ya kupunguza uwezekano wa kuenea kwa maradhi hatari ya mfumo wa upumuaji ya Covid-19.

“Wakati huu ni wa kutafuta mbinu zote kuona ya kwamba tunazuia maambukizi hayo kwa njia yoyote ile. Tunawahimiza wananchi na wakazi wengine popote walipo wafuate sheria, masharti, kanuni na utaratibu wote uliowekwa kuhusu kusafisha mikono ili tupambane na janga hilo,” alisema Bw Kinya.

Alisema katika awamu ya kwanza wataweka vituo 42 katika kaunti ndogo ya Thika huku kila kituo likiwa na mhudumu mmoja wa kuwahamasisha wananchi jinsi ya kunawa mikono kwa njia safi.

“Maeneo muhimu tunayolenga kuwafikia wananchi ni katika masoko, hospitali, na vituo vya magari. Tungetaka wananchi popote pale walipo kushirikiana na wahudumu hao,” alisema Bw Kinya.

Alisema vituo muhimu vinavyolengwa ni hospitalini, vituo vya magari, na sokoni na pahala penginepo ambapo kuna watu wengi.

Baadhi ya washika dau wengine walioungana na kampuni hizo mbili kuendeleza mradi huo ni kampuni ya Chania Travellers, Visha Oshwal, Mama Millers, na Broadway Ltd.

Broadway walitoa matangi 10 ya maji ambayo yanahifadhi lita 2,500 kila moja.

Nayo Chania Travellers Sacco iliwasilisha hundi ya Sh10,000 ili kusaidia mpango huo wa kusambaza maji kwa wananchi.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi, Bw Douglas Mutai, aliwashauri wananchi waepuke misongamano.

“Kusongamana pamoja ni njia moja ya kueneza Covid-19 na hivyo ni muhimu kila mmoja awe mbali kiasi na mwenzake,” alisema Bw Mutai.

Alisema tayari ameagiza maeneo ya burudani na mikahawa ifungwe ili kupunguza mkusanyiko wa watu.

Aliishauri kampuni ya Thiwasco kuhakikisha maji yanasambazwa kwa wingi katika kila eneo ili kukabiliana vyema na virusi hatari vinavyosababisha ugonjwa huo hatari.

Aliwashauri pia wananchi wamrejelee Mwenyezi Mungu ili aweze kuangamiza janga hili ambalo lmekuwa tisho kubwa kwa ulimwengu kwa jumla.

“Wananchi ni sharti wajiweke tayari kwa maswala mazito yaliyo mbele yao. Tusiweke mzaha katika janga hilo,” alisema afisa huyo.

Mwakilishi wa kampuni ya Bidco Bw Willys Ojwang’ alisema kampuni hiyo ilichukua hatua hiyo kwa sababu inaamini kutumikia jamii kwa jumla.

“Sisi Bidco tumejumuika pamoja na Thiwasco Company Ltd kwa lengo la kusaidia jamii pana,” alisema Bw Ojwang’.

Meneja wa biashara na maendeleo katika benki ya Equity tawi la Thika, Bw Sammy Karanu aliwasilisha hundi ya Sh100,000,ili kusaidia kuendeleza mpango wa kusambaza maji kwa wananchi mjini Thika.

“Sisi benki ya Equity tunashirikiana pamoja na washikadau wengine kuona ya kwamba tunawajali wakazi. Licha ya kuweka fedha zao za matumizi ni sharti pia tujitokeze wakati wa shida kusaidia,” alisema Bw Karanu.

  • Tags

You can share this post!

Hofu ya walimu kuhusu mishahara yao na wanafunzi Covid-19...

TANZIA: Kenya yaripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa...

adminleo