• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Bidco Africa yashirikiana na wanawake kibiashara

Bidco Africa yashirikiana na wanawake kibiashara

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Bidco Africa Ltd imetia saini mkataba baina yake na wafanyabiashara wanawake kutoka tabaka tofauti kwa minajili ya ushirikiano.

Wafanyabiashara kutoka sekta tofauti wapatao 100 walikongamana Ijumaa katika makao ya kampuni ya Bidco Africa mjini Thika ili kutafuta mbinu mwafaka jinsi ya kujipanua kibiashara.

Hafla hiyo ya siku moja ilijumuisha wanawake kutoka jijini Nairobi na miji mingine huku lengo lao kuu likiwa kupata ushauri zaidi jinsi ya kupanua biashara na kujitegemea kwa njia ya kipekee.

Mwenyeki wa kampuni hiyo na pia mmiliki wake Dkt Vimal Shah alikuwa mstari wa mbele kuwahamasisha kuhusu hali ya biashara na jinsi ya kusalia kwenye sekta hiyo kwa muda mrefu.

“Mimi binafsi nimekuwa katika ulingo wa biashara kwa zaidi ya miaka 35 lakini safari hiyo haijakuwa mwendo rahisi. Ni kwa sababu ya kujiamini na kuwa na maono sisi kama familia ndiposa tumeweza kufika mahali tulipo sasa,” alisema Dkt Shah.

Aliwahimiza wanawake hao wawe na mipango maalum na maono ili kuafikia malengo yao katika biashara zao.

“Kila mara unapoendesha biashara ni lazima uelewe ni bidhaa ipi wateja wanatamani sana na hiyo ndiyo unayostahili kuweka kwenye soko. Sio vyema kutengeneza bidhaa nyingi zisizohitajika na mteja wako kwa vile utashtukia ukiuza bidhaa hizo kwa bei ya chini wateja wakiwa wachache,” alishauri wanawake hao.

Alisema yeye kama gwiji wa biashara kwa muda mrefu atashirikiana na wao kwa kuwapelekea biadhaa za Bidco Afrika katika makazi zao ili wauzie wateja sehemu hizo.

“Hiyo ni njia moja ya kupanua biashara kwa njia moja ama nyingine huku kila upande ukinufaika. Biashara huanza kwa chini ikielekea hadi juu,” alifafanua Dkt Shah.

Mwenyekiti wa Bidco Africa Ltd Dkt Vimal Shah akiwahamasisha wanawake waliohudhuria kongamano la kibiashara mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Alieleza kuwa amebobea katika biashara kwa muda huo wote kwa kuajiri wataalam walio na ujuzi na wale ameamini wanamsaidia kuendesha kiwanda hicho kwa uwazi.

Bidco imepiga hatua ambapo ina matawi yake katika nchi 38 barani Arika na bado inaendelea kuuza bidhaa mpya za maji ya sharubati aina ya Jooz, Planet, na chakula cha kuku.

Wanawake hao waliohudhuria hafla hiyo wanatoka katika kampuni tofauti kama Kalabasha Investment, SBM Bank, Azzer Supplies, Stemax Ltd, Heri Homes, na Safaricom Ltd.

Wote waliouliza maswali ya kibiashara walijibiwa kwa uwazi huku wakiridhika na majibu hayo.

Baadhi ya wasimamizi wakuu wa kampuni hiyo waliokuwa mstari wa mbele kujibu maswali mazito yaliyoelekezwa upande wao ni, Chrs Diaz, Willis Ojwang’, John Lawrence, John Kariuki, Pritesh Chabhadiya, na Joyce Nzuki.

Baadhi ya maswala muhimu yaliyoangaziwa kuhusu biashara zinazodidimia ni kutokuwa makini kuelewa jinsi ya kujipanga, na kukosa kutafuta ushauri mwafaka kabla ya kuanzisha biashara yoyote.

  • Tags

You can share this post!

KEBS kusaka vipodozi hatari vinavyouzwa nchini

RIZIKI: Wanjiru sasa afurahia bidii yake katika uwekezaji

adminleo