Bidco yawapa wakazi wa Kiandutu sabuni na vyakula
Na LAWRENCE ONGARO
KAMPUNI ya Bidco Africa Ltd inaendelea kutoa msaada kwa wakazi wa Kiandutu mjini Thika.
Kampuni hiyo ikishirikiana na wakfu wa Susan Gitau Counselling Foundation, imetoa msaada huo Jumatatu nje ya kituo cha polisi cha Kiandutu.
Dkt Susan Gitau aliyekuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba wakazi hao wanapokea misaada hiyo, ameishukuru kampuni hiyo kwa ukarimu wake wa kuwajali wasiojiweza.
“Leo kampuni hii imejitolea na kupeana sabuni, mafuta ya kupitia na vyakula tofauti kwa familia zipatazo 1,000 katika kijiji hiki cha Kiandutu,” amesema Dkt Gitau ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nazarene, na mshauri wa kisaikolojia.
Amesema msaada huo utatolewa kwa familia zisizojiweza kabisa kwa utaratibu unaostahili.
“Shughuli hiyo ya kugawanya bidhaa hizo itasimamiwa rasmi na polisi wa kituo cha Kiandutu ili kuwe na uwajibikaji mwafaka,” amesema Dkt Gitau.
Wakati huo pia kampuni ya Bidco imetoa mitungi 20 ya maji za kunawa mikono na pakiti 12 za jeli ya kusafisha mikono ili kuwekwa katika vituo kadha katika kijiji hicho.
Ametoa mwito kwa wakazi hao kufuata maagizo yote ya serikali ili tuweze kupambana na janga hilo la Covid-19.
Afisa wa maswala ya kilimo katika kampuni ya Bidco Africa Ltd, Bw John Kariuki alisema kampuni hiyo imejitolea mhanga kusaidia wasiojiweza kila Mara wakiagizwa kufanya hivyo.
Alisema kampuni hiyo ilijitolea kutoa sabuni, mafuta ya kupitia, na vyakula vitakavyowanufaisha wale walioadhirika.
” Kampuni hii itazidi kushirikiana na wahisani wote popote walipo na njia njema kwa kusaidia wasiojiweza,” alisema Bw Kariuki.
Bw Joseph Mugeto mzee wa nyumba kumi katika kijiji hicho, aliipongeza Bidco Africa Ltd kwa kujali walioathirika na kuwahimiza wazidishe ukarimu huo.
” Sisi kama wakazi wa kijiji hiki tunashukuru hatua uliochukuliwa na Bidco kwani hiyo ni njia moja ya kujali mwanadamu wa chini,” alisema Bw Mugeto.
Alisema kafyu iliyowekwa na serikali imewaathiri wananchi kwa kiwango kikubwa ambapo watu wamekosa pesa na chakula.
Alisema bidhaa zilizotolewa zitafikia kila mmoja anayehitaji msaada huku wakitarajia kutumia haki kwa kila mmoja.
Alitoa mwito kwa wahisani wengine popote walipo wafuate mfano wa Bidco Africa ili kila mmoja aweze kutambulika.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maafisa wakuu wa Bidco Bw Lawrence ‘ Lorezo’ John, Bw Willys Ojwang’ wote walio katika idara ya mauzo, na maafisa wengine waliioandamana nao.