Bidcoro yazindua sharubati aina ya SunQuick
Na LAWRENCE ONGARO
KAMPUNI ya Bidcoro Africa ambayo ni biashara kati ya Bidco Africa na Coro ya nchini ya Denmark, imezindua sharubati aina ya SunQuick.
Kinywaji hicho kipya ni cha kuuzwa katika mataifa ya nje, lakini kiasi kingine kikiuzwa hapa nchini.
Hafla hiyo iliyofanyika Ijumaa wiki jana ilihudhiriwa na Waziri wa Ustawishaji Viwanda na Biashara Bi Betty Maina, pamoja na maafisa wengine mashuhuri wa serikali.
Mwenyekiti wa Bidco Africa Ltd, Vimal Shah, alipongeza serikali kufanikisha uzinduzi huo kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara hapa nchini.
“Ni jambo la kupongezwa hasa wakati huu tunapopambana na janga la Covid-19 ambalo limesababisha viwanda vingi kufungwa. Hata hivyo, kampuni yetu ya Bidcoro Africa Ltd inaendelea kunawiri,” alisema Bw Shah.
Alisema mafanikio yoyote ya kibiashara yanapatikana tu kutokana na bidii, maono, na kujiamini kuwa “inawezekana.”
Alisema janga la corona limeathiri uchumi katika ulimwengu mzima na kwa hivyo ili kujikwamua katika hali hiyo, ni vyema kuja na mbinu mpya ya kibiashara.
“Tutazidi kushirikiana pamoja na mataifa mengine ulimwenguni ili tuafikie malengo yetu. Hiyo inatokana na mazingira thabiti nchini,” alifafanua mwenyekiti huyo.
Bi Betty Maina alisema serikali itatumia takribani Dola 5 bilioni kuendeleza biashara hapa nchini.
“Hata ingawa tuko katika wakati mgumu, serikali inafanya juhudi kuona ya kwamba mambo yanakuwa sawa katika biashara,” alisema Bi Maina.
Alisema nchi ya Kenya inaalika wawekezaji wengi hapa nchini ili kuboresha uchumi wetu.
Aliongeza kuwa bidhaa hiyo ya sharubati itapata wanunuzi wengi hasa katika nchi za nje kutokana na ubora wake.
Afisa mkuu wa maswala ya kibiashara katika benki ya Equity Bw Polycap Igathe alipongeza juhudi za kampuni ya Bidcoro za kushirikiana na Denmark ili kutoa bidhaa mpya katika soko.
Alisema benki ya Equity itazidi kushirikiana na kampuni hiyo kwa maswala muhimu ya kibiashara.
“Sisi kama washikadau katika maswala ya kifedha tuko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wote walio na maono kama yetu,” alisema Bw Igathe.
Alisema Equity kama wawekezaji watafanya juhudi kuona ya kwamba wanashirikiana na watu wanaoendesha biashara zinazotambulika.