• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Binti yangu na mwanawe waliteketea ndani ya nyumba, sikuweza kuwaokoa

Binti yangu na mwanawe waliteketea ndani ya nyumba, sikuweza kuwaokoa

NA JOHN NJOROGE

Mnamo Januari 20, 2024 kilichokuwa usiku wa vicheko na mazungumzo ya kufurahisha kati ya baba, binti na mjukuu kiligeuka kuwa janga nyumbani kwa James Macharia huko Molo, Kaunti ya Nakuru.

Saa chache baadaye, Beatrice Wairimu Macharia, 24, na bintiye Angel Wairimu, 8, walifariki kutokana na moto mkali ndani ya nyumba eneo la Umoja Casino.

Baba mwenye huzuni anapotafakari matukio ya Jumamosi usiku, sasa amebakia tu na kumbukumbu ya mazungumzo ya mwisho na bintiye ambaye angesafiri kwenda Nairobi kwa kazi Jumatatu iliyofuata.

Beatrice Wairimu Macharia, 24.

Angel Wairimu, 8.
Waombolezaji wazidiwa na majonzi kufuatia mkasa wa moto ulioangamiza Beatrice na Angel mtaani Umoja-Casino, Molo. Picha Zote| John Njoroge

Beatrice na Angel walizikwa katika kaburi moja kwenye makaburi ya Molo siku ya Jumatano katika ibada ya mazishi iliyojaa huzuni.

Beatrice, ambaye alipata kazi Nairobi, alikuwa amejadili mipango yake na familia yake kabla tu ya kwenda kulala siku hiyo ya mkasa.

Tulikuwa na mazungumzo ya kupendeza ya baba, binti na mjukuu.  Binti yangu, ambaye ni mtoto wetu wa pili kuzaliwa, alieleza kuwa alipaswa kuripoti kazini Nairobi na nikampa baraka zangu.

“Lakini kama mzee, usingizi ulinipata na nikaenda kulala na kuwaacha nyuma,” Macharia, baba wa watoto watano alieleza.

Kulingana na Macharia, kulitokea hitilafu ya umeme usiku huo na kumfanya bintiye kutumia mshumaa unaoaminika kuwasha moto huo saa kadhaa baadaye na kusababisha maafa.

Mwendo wa saa nane usiku, Macharia anasema aliamshwa na harufu kali lakini hakuweza kujua ilikuwa inatoka wapi.

“Niliangalia sebule na kila kitu kilikuwa sawa lakini nilipofika chumba cha kulala cha watoto, kilikuwa kimejaa moshi.  Niliita jina la Wairimu, binti yangu lakini hakujibu. Nadhani alisahau kuzima mshumaa walipoenda kulala,” alisema.

Akisimulia jitihada za kuwaokoa wapendwa wake waliokuwa wamenaswa kwenye moto huo, Macharia alieleza kuwa alijaribu kuuvunja mlango lakini kishindo cha moto kilikuwa na nguvu sana kwake.

“Ilitubidi tu kupiga mayowe na mke wangu, tukiwavutia majirani ambao walijaribu kutusaidia kuzima moto,” alisema.

Katika simulizi ya kuhuzunisha ya dakika za mwisho za baba akiwa na mtoto wake na mjukuu wake, Macharia aliwaacha waombolezaji wakibubujikwa na machozi zaidi alipokuwa akielezea hali ya kutojiweza.

“Alikuwa mtoto mzuri, mnyenyekevu, mchapakazi na kupendwa na kila mtu katika familia.  Nyaraka zote alizokuwa ametayarisha kwa ajili ya kazi hiyo zote ziliteketea kwa moto ule.  Tumesikitishwa sana na vifo hivyo lakini Mungu atuponye hata baada ya kutuepusha na moto huo,” alisema.

Mkuu wa polisi wa Molo Timon Odingo alisema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo mbaya.

Wakazi wa Molo walielezea wasiwasi wao kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara katika eneo hilo na kuitaka Kenya Power kuongeza transfoma za ziada ili kuzuia majanga sawia.

“Kukatika kwa umeme katika eneo hili kumesababisha hasara ya vifaa vya nyumbani, ikiwa ni pamoja na hii ya hivi majuzi ambapo tumepoteza mwanamke na bintiye,” alisema Peter Muriu, mkazi.

Bw Isaac Njoroge, jamaa wa familia alisema alipofika katika eneo la tukio hakuna lolote lililoweza kufanywa kuokoa maisha ya mama na bintiye kwani tayari walikuwa wamezingirwa na kuuawa na moshi huo.

“Hali ilikuwa mbaya na ilitubidi kuvunja dirisha na kutoa miili. Kwa bahati mbaya, nilipoteza binamu yangu na bintiye,” alisema Bw Njoroge na kuongeza kuwa vitu vingi vya thamani katika chumba hicho viliteketea na kuacha miili pale kitandani.

Alisema kuwa miili hiyo haikuwa imeteketea kiasi cha kutotambulika.

Saa chache baada ya tukio hilo, maafisa wa DCI walifika eneo la tukio na kuondoka dakika chache baada ya kuikagua nyumba hiyo.

Wakati wa mazishi, mwombolezaji mmoja alikashifu kisa hicho lakini akasema huenda watu watano wangeangamia katika kisa hicho cha moto kwani Bw Macharia pamoja na mkewe na mwana wao pia walikuwa ndani ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa mawe wakati wa usiku wa maafa hayo.

“Tunaomba kwamba hakuna familia itakayopoteza wapendwa wao kupitia mkasa kama huo wa moto au kupitia kwa ajali,” akasema kasisi aliyeongoza hafla hiyo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wa Isongo washtakiwa kwa kuvuruga amani shuleni

Ukusanyaji wa mapato Nairobi wasalia ‘pasua...

T L