• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Bintiye Raila asema bado hajabanduka kwa siasa

Bintiye Raila asema bado hajabanduka kwa siasa

Na WANDERI KAMAU

MWANAWE kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Rosemary Odinga amesema kwamba hajaondoka katika ulingo wa siasa licha ya matatizo ya kiafya yanayomkumba.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumapili usiku, Bi Odinga alisema kwamba yuko tayari kuhudumu katika nafasi yoyote itakayopatikana wakati ufaao utakapofika.

“Mimi ni mtu wa watu. Matatizo niliyo nayo si kikwazo hata kidogo cha kunizuia kutowahudumia wananchi. Si mimi wa kwanza kujipata katika hali hii. Kuna viongozi hata wanaowawakilisha watu walemavu,” akasema.

Mwaka uliopita, Bi Odinga alilazimika kukatiza kampeni za kuwania ubunge katika eneo la Kibra kutafuta matibabu kwa maradhi yaliyomwacha akiwa na matatizo ya kuona vizuri.

Ikiwa mara ya kwanza kujitokeza hadharani tangu wakati huo, Bi Odinga alisema kuwa angali anaamini kwamba bado ana nguvu za kukihudumia kizazi chake.

“Babangu (Raila) ni maarufu kwani amekuwa uongozini kwa muda mrefu. Ninaamini nafasi ya kukitumikia kizazi changu ingalipo. Msukumo wangu unatokana na nia ya kuwatumikia watu, ila si umaarufu wa kisiasa wa familia yetu,” akasema.

Akirejelea matatizo yake ya afya, alisema kuwa ilianza kama maumivu ya kawaida ya kichwa, ila yakageuka kuwa tatizo lililomlazimu kukatiza shughuli zote za kisiasa.

“Nilikuwa mjini Naivasha na wanangu wawili wakati nilianza kuhisi maumivu ya kawaida ya kichwa. Hata hivyo, hali ilinizidia. Nilizimia na kuanguka katika chumba nilimokuwa. Nilisafirishwa jijini Nairobi kwa ndege kupokea matibabu ya dharura,” akasema.

Baada ya kuchunguzwa na madaktari, ilibainika kwamba alikuwa na uvimbe katika ubongo.

Alilazimika kusafirishwa nchini Uchina kwa matibabu zaidi. Akiwa humo, uvimbe huo uliondolewa ila hali yake haikuimarika sana.

Ilibidi kusafirishwa nchini Afrika Kusini, alikolazwa katika hospitali moja hadi baadaye mwaka huu aliporejea Kenya.

Bi Odinga pia alikanusha tetesi kwamba amepoteza kabisa uwezo wake wa kuona, akisema kuwa ni jicho lake tu moja ambalo halioni vizuri.

“Ingawa nina ugumu wa kujifanyia baadhi ya mambo ambayo niliyafanya binafsi, hili halimaanishi kwamba siwezi kuona hata kidogo.”

Ninaendelea kutafuta matibabu zaidi ili kurejesha hali yangu ya kawaida,” akasema.

Ujio wa Bi Odinga siasani ulionekana kama mkakati wa mapema wa familia ya Bw Odinga kumtayarisha kama mrithi wake, dhana ambayo amekuwa akiikanusha.

Kabla yake kujitosa siasani, mwanawe Odinga, Fidel Odinga ndiye alikuwa akionekana kama mrithi wa Bw Odinga kabla ya kifo chake mnamo 2015.

Baada ya uchaguzi huo, mbunge wa awali, Kenneth Okoth aliibuka mshindi na kuanza kuhudumu kwa kipindi cha pili.

You can share this post!

IPOA kuchunguza polisi aliyeua watu 5 na kuwajeruhi wengine

Nyota ya kisiasa ya Isaac Ruto yaanza kung’aa tena

adminleo