Binyavanga aombolezwa kama mwandishi shupavu
Na WANDERI KAMAU
WAANDISHI wa vitabu, wanahabari, wanaharakati wa kijamii na kitamaduni jana walituma rambirambi zao kuomboleza kifo cha mwandishi mbishi Binyavanga Wainaina.
Kulingana na mwenyekiti wa Jukwaa la Fasihi, ‘Kwani?’ Tom Maliti, mwandishi huyo alifariki dakika chache baada ya saa nne usiku mnamo Jumanne katika Nairobi Hospital, jijini Nairobi.
Marehemu ambaye, ndiye mwasisi wa jukwaa hilo alifariki akiwa na umri wa miaka 48. Duru kutoka kwa familia yake zilisema alifariki kutokana na kiharusi.
Alikuwa akigonga vichwa vya habari mara kwa mara kutokana na misimamo yake mikali iliyokinzana na tamaduni za Kiafrika. Marehemu alikuwa ametangaza hadharani kuwa ni basha.
Kwenye jumbe zao, waandishi mbalimbali walimsifia kwa mchango wake mkubwa katika ulingo wa fasihi, hali iliyomwezesha kuibuka mshindi kwenye tuzo ya kifahari ya fasihi ya Caine mnamo 2002.
Mwandishi Yvonne Odhiambo Owuor alimtaja kama “mwandani wa karibu ambaye amemwacha mpweke.”
“Usiku mwema, mwandani wangu, usiku mwema. Leo, kesho na mtondo, hakuna jambo litakalonipa ufafanuzi kamili kuhusu sababu ya kifo chako,” akasema mwandishi huyo, kwenye shairi aliloandika kuomboleza kifo hicho.
“Marehemu Binyavanga ameacha pengo kubwa katika tasnia ya uandishi wa kubuni. Kipaji chake kilikuwa cha kipekee,” akasema Dkt Joyce Nyairo, ambaye ni mwandishi na mwanaharakati wa masuala ya kitamaduni.
Mwandishi Kingwa Kamencu, alisema kifo hicho kilimwacha akiwa mwenye majonzi mengi.
“Majonzi yalinijaa nilipoamka na kupata habari za kifo cha mwenzangu Binyavanga,” akasema.
Wengine waliomwomboleza ni wasomi Prof Egara Kabanji, Dkt Wandia Njoya, waandishi Jackson Biko, Oyunga Pala kati ya wengine.
Marehemu alikuwa akizua hisia mseto, kwani hakuogopa kueleza wazi yale aliyoyaamini, ambapo mara nyingi yalikinzana na itikadi nyingi za Kiafrika.
Mnamo 2014, aliwashangaza wengi alipotangaza wazi kuwa ni basha. Alitoa ujumbe huo kwenye makala kubwa aliyoandika katika jarida la Chimurenga Chronicles.
Mnamo 2016, alitangaza kwamba alikuwa na virusi vya HIV, lakini hakuhofishwa na hali yake.
“Nina virusi vya HIV, lakini naendelea na maisha yangu kama kawaida,” akasema.
Mwaka uliopita, alieleza furaha yake kwamba alikuwa akitarajiwa kuolewa na mpenziwe, ambaye ni mwanamume nchini Afrika Kusini mwaka huu.
Mpenziwe ni raia wa Nigeria. Kulingana na marehemu, harusi hiyo ingefanyika Afrika Kusini na Nairobi.
Marehemu, ambaye anasifika kwa uumbuji mkubwa katika kazi zake za kifasihi alizaliwa mnamo Januari 18, 1971 katika Kaunti ya Nakuru. Alisomea katika shule za upili za Mangu’u (Thika) na Lenana (Nairobi). Alisomea katika vyuo vikuu vya Transkei (Afrika Kusini) na East Anglia (Uingereza).
Alipata umaarufu kwa kitabu chake ‘One Day I’ll Write About This Place’ (Siku Moja Nitaandika Kuhusu Mahali Hapa) ambacho kilichapishwa mnamo 2011.
Kando na uandishi, amekuwa akitoa mihadhara katika vyuo mbalimbali duniani kuhusu uandishi wa kubuni.