BONASI DUNI: Wabunge waipapura KTDA
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE watano kutoka kaunti za eneo la South Rift wamemtaka Waziri Kilimo Mwangi Kiunjuri kulainisha sekta ya majanichai kwa kuwaondoa walaghai wanaowapunja wakulima kwa kuwapa malipo duni kwa zao hilo.
Vilevile, wanamtaka Bw Kiunjuri kupiga kampuni za 11 za kuuza zao hilo wakisema ndizo hupata faida kubwa huku wakilima wakiteseka kutokana mapato duni.
“Inasikitisha kwamba mwaka huu KTDA imewalipa wakulima bonasi ya Sh17 kwa kilo moja kutoka Sh60 mwaka 2018. Tofauti kati ya bei hizi mbili ni kubwa zaidi hata ingawa ni kweli kwamba mataifa ambayo yamekuwa yakinunua majani chai kutoka Kenya yanakumbwa na misukosuko,” mbunge wa Buret Japhet Mutai akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano.
Bw Mutai alikuwa ameandakama na wenzake; Brighton Yegon (Konoin), Beatrice Kones (Bomet Mashariki), Dominic Koskei (Sotik), Sammy Saroney (Mbunge Maalum) na Caleb Kositany.
Wabunge hao sasa wanataka Waziri Kiunjuri na wasimamizi wa KTDA wafike mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo watoa ufafanuzi kamilifu kuhusu kushuka kwa mapato ya wakulima.
“Hatutaki KTDA kuendelea kuwanyanyasa wakulima wetu kwa kisingizio cha kushuka kwa bei ya majani chai katika masoko ya kimataifa. Sh17 ambazo wamelipa wakulima mwaka huu haziwezi kukimu mahitaji yao,” akasema Bw Yego.
Akaongeza: “Ikiwa bei ya majanichai imeshuka, KTDA inafaa kugawana hasara hiyo na wakulima.”
Naye Bw Koskei aliitaka serikali kuvunjilia mbali kile alichokitaja kama ukiritimba wa KTDA kwa kutoa leseni ya kununua majani cha kutoka kwa wakulima kwa mashirika mengine ya kibinafsi.
“Tunataka KTDA ipewe ushindani ili iweze kujali masilahi ya wakulima,” akasema.
Wabunge hao pia waliitaka serikali ya kitaifa kuanzisha hazina maalum ya kuwakimu wakulima kutokana na kushuka kwa bei ya majani chai.