Boya lililotoweka baharini lasakwa
NA KALUME KAZUNGU
TAHADHARI inazidi kutolewa kwa mabaharia wote eneo la Pwani kuwa waangalifu wanapoendesha vyombo vyao baharini ili kuepuka kugongana na boya maalum (pontoon) lililotoweka siku tano zilizopopita baada ya kukatika kutoka kwa jeti ya Mtangawanda, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.
Katika ujumbe wake kwa vyomvo vya habari Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Udhibiti wa Vyombo vya Majini (KMA), George Macgoye, alisema msako mkali umeanzishwa baharini ili kubaini lilipo boya hilo.
Alisema KMA inashirikiana na Halmashauri ya Bandari nchini (KPA), Bandari ya Lamu (LAPSSET), Polisi wanaoshughulikia masuala ya Baharini na wale wa mipakani (RBPU) katika kulitafuta boya hilo.
Boya ni kifaa kilichotengenezwa kwa chuma na ambacho kina muundo ulioshabihiana na sanduku na ambacho huelea majini.
Kifaa hicho mara nyingi hufungwa minyororo kwa kushikanishwa na jeti na hutumiwa sana hasa katika kushukisha na kupandishia abiria na mizigo kwenye jeti husika.
Bw Macgoye aliwataka wavuvi, wahudumu wa boti na wasafiri wanaotumia Bahari Hindi eneo la Pwani kuwa macho na kupiga ripoti kwa ofisi ya KMA punde watakapokutana na boya hilo baharini.
“Boya lililotoweka siku tano zilizopita bado halijapatikana hadi sasa. KMA imeshirikiana na KPA, maafisa wa naoshughulikia masuala ya baharini na wale wa RBPU ili kulisaka boya hilo.
Ningewasihi mabaharia, wavuvi na hata wasafiri wanaotumia bahari ya Lamu na Pwani kwa jumla kuwa waangalifu ili kuepuka ajali ambazo huenda zikachangiwa na boya hilo. Tutawajulisha punde boya hilo litakapopatikana,” akasema Bw Macgoye.