Habari Mseto

Bunge kuchunguza madai ya utupaji taka hatari za nyuklia eneo la kaskazini

June 15th, 2024 2 min read

NA EDWIN MUTAI

BUNGE limeanza uchunguzi rasmi kuhusu madai ya utupaji taka za nyuklia na vifaa hatari Kaskazini mwa Kenya.

Kamati ya Bunge ya Mazingira, Misitu na Madini imesema itafanya uchunguzi kamili baada ya Wizara ya Mazingira kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusiana na madai hayo.

“Kufuatia majibu yasiyoridhisha kutoka kwa Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Bi Soipan Tuya, tumeazimia kuanza uchunguzi kamili kuhusu madai hayo,” alisema Mbunge Mwakilishi wa Kike Kwale, Bi Fatuma Hamisi.

“Tutashirikisha wahusika wote ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mazingira, Mambo ya Ndani, Nishati, Petroli, Afya, Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya (Kemri), Taasisi ya Saratani na Taasisi ya Nishati ya Nyuklia katika Chuo Kikuu cha Nairobi miongoni mwa wengine.”

Kamati hiyo ilisema baada ya hapo itafanya kazi ya kutafuta ukweli katika eneo la Kaskazini Mashariki ambapo itashirikisha watu walioathirika, waathirika wa saratani, wanawake na watoto.

“Tutaandamana na wawakilishi wa Wizara zilizotajwa, wataalam wa afya miongoni mwa wengine kutathmini madai ya utupaji taka za nyuklia Kaskazini mwa Kenya. Kunaweza kuwa na athari nyingi sasa kuliko wakati Wizara ilipofanya ripoti hii isiyoridhisha,” Bi Hamisi ambaye aliongoza kikao hicho kwa muda alisema.

Uchunguzi huo unafuatia agizo la Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Moses Wetangula kwa kamati hiyo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo baada ya kupata jibu la Bi Tuya kuwa haliridhishi.

Uchunguzi huo ulichochewa na ombi lililowasilishwa na Bw Mohamed Adow kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya utupaji taka za nyuklia katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na kampuni za kigeni.

Bw Adow aliitaka kamati ya Mazingira, Misitu na Uchimbaji madini inayoongozwa na Mbunge David Gikaria kuchunguza madai kwamba serikali kupitia Wizara ya Nishati iliidhinisha utupaji wa vifaa hatari, ikiwa ni pamoja na taka za nyuklia, mwishoni mwa miaka ya 1980 na 1990.

Anaitaka kamati hiyo kubaini ukweli juu ya madai hayo na kuamua athari zake kwa mazingira na wakazi.

Akijibu Bunge, Bi Tuiya alisema Wizara inafahamu kuwa mwishoni mwa miaka ya 1980 na 1990, serikali ilikuwa imeanza shughuli za kuchimba mafuta katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya, ikijumuisha Kaunti za Wajir na Marsabit.