BURIANI MOI: Alikuwa rais mcha Mungu na hakuwahi kunywa pombe
Na BENSON MATHEKA
RAIS Mstaafu Daniel Toroitch arap Moi alidumisha mtindo wa kipekee wa maisha katika maisha yake ya kisiasa na uongozi na hata alipostaafu. Mzee Moi alikuwa mtu mcha Mungu na inasemekana haikuwa rahisi kuchelewa kwenda kanisani.
Wakati wa utawala wake wa miaka 24, alikuwa akihudhuria ibada katika kanisa la AIC la Kabarak, Nakuru siku za Jumapili. Wakati mwingine aliabudu katika makanisa mbalimbali maeneo tofauti nchini.
Katika maisha yake yote, Moi hakunywa pombe, jambo linalohusishwa na maisha yake marefu na alikuwa akishawishi watu katika serikali yake kuacha pombe.
Inasemekana kuwa hakuvumilia kiongozi au maafisa wa serikali waliobainika kutekwa na ulevi. Inasemekana Moi alikuwa akipenda sana vyakula vya kiasili; alipenda mahindi yaliyochemshwa na uji au chai kama kiamsha kinywa.
Waliofanya kazi naye au chini yake wanasema alikuwa mchapa kazi. Angeamka alfajiri kusoma Bibilia kabla ya kuanza shughuli zake za kila siku.
Moi alikuwa mtu wa kufuata wakati na hakuwa akichelewa katika hafla za kibinafsi, kifamilia na kisiasa. Katika miaka 24 aliyotawala Kenya, Moi hakuenda likizoni. Ni kiongozi aliyependa kutumia muda wake kutembelea maeneo tofauti nchini hasa kukutana na watoto.
Kila eneo alilotembelea alikuwa akipitia shule za karibu kuwasalimia watoto na kuwapa zawadi. Yasemekana akiwa rais, aliwahi kulala kwenye hema mara mbili akiwa maeneo ya mashambani. Moi alipenda kuwatembelea marafiki wake katika maboma yao alipozuru maeneo yao.
Katika kipindi alichokuwa katika utumishi wa umma na rais kwa miaka 24, Moi alijulikana kwa ukarimu wake na inasemekana hadi alipougua na kulazwa hospitalini alikuwa akitumia zaidi ya Sh10 milioni kwa mwaka kusaidia wasiojiweza.
Akiwa Rais, alipalilia mwito wa harambee, ambazo alikuwa akitumia kujivumisha. Ni kupitia harambee ambapo shule nyingi na hospitali zilijengwa. Moi alikuwa akipenda wageni na alipokea jumbe mbalimbali kila wakati katika ikulu au nyumbani kwake Kabarak, Nakuru.
Inasemekana Moi alikuwa na fundi mmoja aliyeshona suti zake zote alipokuwa mamlakani.