BURIANI MOI: Aliwakabili vikali watu waliokosoa utawala wake
Na WANDERI KAMAU
RAIS Mstaafu Daniel Moi atakumbukwa kwa kuwakabili vikali wale ambao walikosoa utawala wake.
Miongoni mwa waliojikuta kwenye mkwaruzano wa kisiasa na Mzee Moi ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo, mfanyabiashara Andrew Muthemba, wanachama wa kundi la Mwakenya, kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwanasiasa Kenneth Matiba, Kaasisi Timothy Njoya kati ya wengine.
Masaibu ya Bw Njonjo, yalianza kwenye mkutano mmoja wa Bw Moi Kaunti ya Kisii mnamo 1983. Kwenye ziara katika eneo hilo, Bw Moi alisema kuwa baadhi ya nchi za ng’ambo zilikuwa zikipanga kumsaidia mmoja wa “wasaliti wake” kutwaa uongozi.
Muda mfupi baada ya mkutano wa Kisii, mbunge wa Kericho ya Kati Francis Mutwol alimtaja Bw Njonjo kuwa msaliti aliyepania kutwaa mamlaka ya rais.
Kilichofuatia kilikuwa msururu wa matukio ya kumhangaisha Bw Njonjo, hali iliyomfanya kujiuzulu cheo cha Waziri na Mbunge.
Mnamo Juni 29, 1983, mbunge wa Butere Martin Shikuku aliwasilisha stakabadhi Bungeni akidai kwamba Bw Njonjo alimiliki biashara za siri nchini Afrika Kusini, na alikuwa ameingiza silaha hatari nchini kinyume cha sheria ili kuipindua serikali.