BURIANI MOI: Bendera kupeperushwa nusu mlingoti
Na DIANA MUTHEU
RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza bendera ya Kenya ipeperushwe nusu mlingoti kuanzia jana hadi atakapozikwa aliyekuwa Rais wa Pili Daniel arap Moi.
Akituma rambirambi zake kwa ndugu jamaa na marafiki wa Mzee Moi, Rais alisema bendera katika ikulu, majengo yote ya serikali, maeneo yote ya umma, vituo vyote vya polisi, kambi za jeshi na vyombo vyote vya majini vinavyotumiwa na jeshi zitapeperushwa nusu mlingoti.
Pia, bendera katika majengo ya balozi za Kenya katika mataifa ya kigeni zitapeperushwa nusu mlingoti.
“Bendera hizo zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia saa kumi asubuhi mnamo Februari 4 hadi baada ya Mzee Moi kuzikwa,” akasema Rais.
Rais Kenyatta alisema kuwa nchi nzima itaomboleza kifo cha Mzee Moi hadi pale atakapozikwa kama njia ya kuonyesha heshima kwa mwendazake.
Viongozi mbalimbali na hata wananchi walituma rambirambi zao kupitia mitandao mbalimbali za kijamii kama vile Twitter, Whatsapp na Facebook.
Rais Kenyatta alimtaja Mzee Moi kama kiongozi aliyejitolea kuhudumia wakenya katika vyeo vyote alivyochaguliwa na kuwa nchi imempoteza mtu wa maana sana.
“Alihudumia Wakenya kama mwalimu, mwanasheria, mbunge, waziri, makamu wa rais kisha akawa rais,” akaeleza Rais Kenyatta.