Habari Mseto

Bwanaharusi aliyeachwa kwa mataa ataka watu wasikate tamaa katika suala la mapenzi

February 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na VITALIS KIMUTAI

AMOS Rono, mwanaume ambaye harusi yake ilitibuka mwaka jana baada ya kuachwa na mpenziwe, jana alitumia siku ya kuwasherehekea wapendanao kuwashauri vijana wasikate tamaa mambo ya mahaba yanapowaendea mrama.

Harusi ya Bw Rono ilikosa kufanyika mnamo Disemba 9 mwaka jana, baada ya mchumba wake Nelly Chepkoech Koskei kughairi nia na kumhepa dakika za mwisho.

Jana, Bw Rono alisherehekea siku ya wapendanao akiwa na upweke na kimya kingi katika kijiji chao cha Kapsoiyo, Kaunti ya Bomet.

Alikuwa amepanga angalau mwaka huu angesherehekea Valentino na mkewe lakini mambo yakakosa kuenda jinsi alivyopanga.

Jana, alikuwa akitafakari kuhusu maisha yake na jinsi Mungu amemrehemu baada ya tukio hilo.

“Iwapo harusi yangu ingefanikiwa, leo ningempeleka mchumba wangu katika hoteli tule chajio huko. Nafasi hiyo sasa inasubiri mtu ambaye atakuwa mke wangu,” akasema Bw Rono.

Licha ya kuandamwa na wanawake lukuki ambao wanataka aingie nao kwenye ndoa, Bw Rono anasema kwa sasa anatafuta kazi ya kudumu kabla hajaamua kuingia kwenye ndoa.

“Nilivunjika moyo na nikaathirika sana kisaikolojia. Iwapo hamngeniunga mkono na kunisaidia kimawazo, huenda ningekuwa hata nimejiangamiza,” akaongeza.

Kutokana na wanawake wengi ambao wamekuwa wakimsaka awaoe, imebidi abadilishe nambari yake ya simu ila bado wanamsaka.

“Simtafuti mpenzi kwa sasa, bado naendelea kupona roho kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa. Sijafunga mlango wa kuingia kwenye uhusiano mwingine ila bado nachukua muda wangu,” akasema.

“Wale ambao wananiandama wasikate tamaa kwa sababu siku moja nitafanya uamuzi na huenda mmoja wao akabahatika,” akasema.

Kuhusiana na harusi iliyotibuka, mwanaume huyo alifichua kuwa hajaongea na aliyekuwa mchumba wake. Pia alisema hana mpango wowote wa kuendea mahari aliyotoa ya ng’ombe watano.

“Hili ni suala ambalo wazee ndio watalishughulikia. Sina wajibu wowote wa kutekeleza kuhusu hilo. Mambo haya yatashughulikiwa kulingana na tamaduni ya jamii ya Kipsigis.”

Tangu kutibuka kwa harusi hiyo, Bw Rono amekuwa akitoa ushauri kuhusiana na changamoto mbalimbali kwenye mahusiano.

Amekiri kuwa mwanzoni hakuamini mchumba wake alimwaacha ila nasaha alizopata na ushauri kutoka kwa wengi, zilimsaidia kuendelea na maisha yake.

Kutibuka kwa harusi hiyo iliyotarajiwa kufanyika katika kanisa la Kapsoiyo African Gospel ndio iliwafanya wakajulikana sana baada ya kugonga vichwa vya habari.

Kuhusu siku ya wapendanao, Bw Rono aliwashauri wanandoa kuvumiliana ili kukabili changamoto pamoja na kuzitumia kusaka maisha mazuri.

“Mapenzi yanastahili kuwa ya ukweli na wanandoa au wapenzi hawafai kutiana shinikizo tele. Badala yake wavumiliane na kukwea ngazi ya maisha bila tafrani zozote,” akaongeza Bw Rono.