Caroline Mwatha aliuawa na polisi – Orengo
NA CAROLINE MUNDU
VIONGOZI katika Kaunti ya Siaya, wamepuuzilia mbali ripoti ya uchunguzi wa polisi iliyoonyesha mwanaharakati Caroline Mwatha aliaga dunia kupitia uavyaji mimba.
Wanasiasa hao pamoja na familia ya marehemu, sasa wanataka uchunguzi wa kina kufanywa ili kutegua kitendawaili cha kilichomuua mwanaharakati huyo, aliyefahamika sana mtaani Dandora kwa kuwatetea raia.
Wakiongozwa na Seneta James Orengo, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Dkt Christine Ombaka, Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo na mwenzake wa Gem, Elisha Odhiambo, viongozi hao walikemea matokeo ya uchunguzi wa polisi wakati wa mazishi ya mwanaharakati huyo katika kijiji cha Asembo, eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya.
Bw Orengo alisikitika kwamba mauaji ya kiholela ya wanaharakati na kupotea kwa watu kwa njia tatanishi yanaendelea kuongezeka kwa kiwango cha kutisha nchini, huku polisi wanaohusika wakisalia huru bila kuchukuliwa hatua.
“Tunataka majibu kuhusu kifo cha Bi Mwatha. Hatujaridhishwa na uchunguzi uliofanywa na polisi kuhusu kifo cha mwanamke huyu. Tabia ya polisi kuwatekea wanaharakati kisha kuwaua kwa njia tatanishi lazima ikome,” akasema Seneta Orengo.
“Hatujasahau jinsi marehemu Musando alivyouawa kinyama. Tunawaambia polisi kuchunguza visa hivi kwa makini kabla hawajazungumza kuvihusu,” akasema.
Matamshi ya seneta huyo yaliungwa mkono na Bw Odhiambo, ambaye aliwataka polisi kufuata sheria badala ya kutoa ripoti aliyosema inaficha ukweli kuhusu mauaji ya Bi Mwatha.
“Walioshiriki mauaji ya msichana huyo lazima waadhibiwe kisheria, na ikiwa ni polisi waliohusika, nawalaani kabisa. Lazima tuheshimu uhai wa binadamu wenzetu,” akasema Bw Odhiambo.
Mumewe marehemu, Joshua Ochieng’ ambaye alizidiwa na hisia wakati wa ibada ya mazishi, alimtaja mkewe kama shujaa atakayekumbukwa na wengi.
“Nimempoteza rafiki na mke. Alikuwa shujaa atakayekumbukwa sana,” akasema Bw Ochieng’ akidondokwa na machozi.
Stanslaus Mbai, babake Bi Mwatha alisema mwanawe hakuwa mjamzito na kudai kwamba alikatwa tumboni kisha kijusi kikawekwa ndani.