CCTV zaidi jijini, Moi Avenue kutumiwa na magari ya upande mmoja
Na BERNARDINE MUTANU
Serikali ya Kaunti ya Nairobi itasakini kamera mpya za CCTV na mataa katikati mwa jiji kwa lengo la kuimarisha usalama.
Vile vile, serikali imeajiri maafisa zaidi wa kudhibiti trafiki ambao watasimama katika makutano yote ya barabara Jijini kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari masaa ya asubuhi na jioni.
Afisa anayesimamia uchukuzi Nairobi Mohamed Dagane alisema baraza la jiji pamoja na Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imebudi kamati ya uchukuzi na usalama Nairobi kuambatana na Sheria ya NTSA, 2012 kwa lengo la kukabiliana na ukosefu wa usalama.
Bw Dagane alisema kaunti imepiga marufuku waendeshaji wa boda boda katikati mwa jiji. Kutokana na hilo, maafisa wa usalama wa kaunti wanawakamata bodaboda wanaohudumu humo.
Kulingana naye, waendeshaji wa boda boda wametishia usalama wa jiji zaidi ya kuwa wameongeza msongamano jijini.
Afisa huyo alisema kuwa serikali ya kaunti ina mpango wa kuifanya Barabara ya Moi Avenue kutumiwa na magari yanayoelekea upande mmoja kwa lengo la kupunguza trafiki itakayoibuliwa na kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Bus Rapid Transit (BRT).