• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Chaguo la mambo matatu la Rais laleta afueni sekta ya miwa ikiimarika  

Chaguo la mambo matatu la Rais laleta afueni sekta ya miwa ikiimarika  

NA BRIAN AMBANI

KIWANGO cha sukari inayoagiziwa nchini kimepungua kufuatia kuimarika kwa uzalishaji nchini, huku viwanda vikirejelea shughuli baada ya miezi kadhaa ya kufungwa kutokana na uhaba wa miwa.

Kulingana na Data kutoka kwa Idara ya Sukari, wafanyabiashara waliagiza kutoka nchi za kigeni tani 42,381 za sukari mwezi uliopita, kiasi ambacho ni cha chini zaidi tangu Julai 2023, ambapo tani 27,179 za bidhaa hiyo ziliagiziwa.

Kenya haikuagizia sukari katika muda wa miezi mitatu iliyopita baada ya serikali kufuta marufuku ya miezi mitano iliyodhamiriwa kukomesha usagaji wa miwa ambayo haijakomaa.

Marufuku hiyo iliondolewa Desemba kufuatia kukomaa kwa miwa ya kutosha ambayo imefufua viwanda vya sukari.

Wakati wa marufuku hiyo, wenye viwanda walijaribu bila mafanikio kuitaka serikali iwaruhusu kuagiza bidhaa hiyo wakihoji wamebuni mitandao ya usambazaji bidhaa ikilinganishwa na wafanyabiashara.

Viwanda vya humu nchini vilisaga tani 63,075 za sukari mwezi uliopita, kiasi ambacho ni cha juu zaidi cha bidhaa hiyo tangu Januari 2023.

“Kwa jumla sukari iliyozalishwa (kupakiwa kwenye mifuko) Februari 2024 ilikuwa tani 63,075 nyongeza ya asilimia nne kutoka tani 60,680 zilizorekodiwa mwezi uliotangulia,” ilisema Idara ya Sukari.

Kufunguliwa tena kwa viwanda vya sukari kumesababisha bei za bidhaa hiyo kushuka pakubwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na kuwapiga jeki wateja.

Mumias Sugar, ni mojawapo ya viwanda ambavyo serikali ya Rais William Ruto imeweka mikakati kufufua utendakazi.

Aidha, kampuni hiyo ilifungua milango yake kuanza kuhudumu tena mnamo Desemba 1, 2023.

Ilikuwa imesalia kufungwa tangu mwaka 2020.

Wakulima wa miwa wamekuwa wakilalamikia malipo duni, ikiwemo kupunjwa hela kwa kukosa kulipwa wanaposambazia viwanda vya miwa.

Dkt Ruto, hata hivyo, ameapa kukabiliana na mawakala walioteka nyara sekta ya sukari nchini, huku akiahidi kuhakikisha kilimo cha miwa kinafufuliwa.

Mwaka uliopita, 2023, Rais alijipata akikosolewa vikali kufuatia vitisho vyake kwa matapeli katika sekta ya miwa ambapo alitumia maneno haya, “wachague mambo matatu; wahame Kenya, waende jela au nitawapeleka mbinguni”.

  • Tags

You can share this post!

Kesi yako ilikuwa stori za ‘jaba’, korti...

Al-Shabaab warudisha kilimo cha zingifuri kuwa...

T L