Habari Mseto

Chama cha ushirika cha Urithi Premier Sacco chabadilisha jina

October 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha ushirika cha Urithi Premier Sacco (UPS), tayari kimefanya mabadiliko na kujiita Anchor Premier Sacco ili kujiuza kwa kwa njia mpya kabisa.

Mwenyekiti wa Urithi Housing Cooperative Sacco Ltd, Bw Samuel Maina alisema msimamo huo uliafikiwa baada ya vyama viwili vya ushirika; Urithi Premier Sacco na Urithi Housing Cooperative ambavyo vimekuwa vikiendesha shughuli zao kwa pamoja, lakini wateja wengi wakionekana kutotafautisha pande hizo mbili.

“Tulifanya kikao na tukaafikiana upande mmoja wa mrengo huo ubadilishe jina ili pia kuboresha hali yake ya kibiashara,” alisema Bw Maina.

Mwenyekiti wa Urithi Housing Cooperative Sacco Ltd Bw Samuel Maina akihutubia wanachama wake mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Alitaja umma na wawekezaji wengi kama miongoni mwa wale waliokosa kutofautisha mirengo hiyo miwili.

Hata hivyo aliwajulisha wateja wake kuwa Chama cha Urithi Housing Cooperative Ltd bado kitaendelea kuhudumia wateja wake kikiwa na jina hilo.

“Kwa hivyo ni vyema kusisitiza kuwa mabadiliko ni kwa Chama cha ushirika cha Urithi Premier Sacco (UPS) kuitwa Anchor Premier Sacco (APS),” alisema Bw Maina.

Kujadiliana kwa kina

Aliyasema hayo Jumanne mjini Thika alipokutana na wanachama wake ili kujadiliana kwa kina kuhusu mabadiliko hayo.

Alisema kila mrengo utaendelea kutoa huduma zake kama hapo awali ilivyopangwa.

“Kwa mfano, chama cha Urithi Housing Cooperative Society kitaendelea kuuza ardhi na majumba jinsi ilivyoratibiwa. Halafu wenzetu wa Anchor Premier Sacco Ltd wataendelea kutoa mikopo ya kifedha kwa wateja wake,” alisema Bw Maina.

Aliwahimiza wanachama wazidi kuwa na imani na vyama vyote viwili kwa sababu wao kama viongozi wako tayari kuwatumikia bila ubaguzi wowote.

Alisema kwa upande wao, wamewekeza pahala pengi kote nchini ambapo baadhi ya maeneo walikofika ni Pwani, Thika, Ruiru, na Nakuru.

“Lengo letu pia ni kufuata ajenda nne kuu za serikali zikijumuisha ujenzi wa makazi; ambao tunaendeleza,” alisema Bw Maina.

Aliwahimiza wanachama wote popote walipo wawe mstari wa mbele kukikumbatia chama chao ili kiweze kuboreshwa zaidi.