Habari Mseto

Chang'aa ni dawa ya homa ya matumbo, mshtakiwa aambia hakimu

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

Mwanamume Jumatano alizua kicheko katika mahakama ya Kibera, Nairobi kwa kudai kwamba chang’aa huwa inamsaidia kuzima makali ya homa ya tumbo.

Bw Linus Odhiambo aliambia Hakimu Mkuu Joyce Gandani kwamba lita mbili na nusu za chang’aa alizopatikana nazo ni dawa ya kutibu homa ya matumbo.

“Mheshimiwa, ni kweli nilipatikana na chang’aa ninayotumia kama dawa ya tumbo. Huwa inanisaidia sana kuzima maumivu ya homa ya tumbo ambayo huwa inanisumbua sana,” Bw Odhiambo alieleza mahakama.

Alisema alipatikana na kiwango kidogo cha pombe hiyo haramu lakini akakanusha kwamba alikuwa katika harakati za kuiuza.

“Haikuwa ya kuuza, ilikuwa dawa tu,” alisema.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulisema kwamba pombe hiyo ilikuwa haramu na haikuwa imepakiwa kulingana na sheria.

“Mshtakiwa alipatikana na lita mbili na nusu za pombe ya chang’aa ambayo haikuwa imepakiwa inavyohitajika kisheria. Pombe hiyo ilikuwa kwenye chupa,” alieleza kiongozi wa mashtaka Zafida Chege.

Alipoonyeshwa chupa iliyokuwa na pombe hiyo, Bw Odhiambo alisema polisi waliiongeza.

“Yangu haikuwa nyingi hivi, hata hivyo ni kweli nilikuwa na chang’aa ninayotumia kama dawa,” alieleza.

Mahakama iliambiwa kwamba alitenda kosa hilo katika eneo la Kabete jijini Nairobi Juni 17 mwaka huu. Alitozwa faini ya Sh5000 au afungwe jela miezi mitatu akikosa kulipa faini hiyo.