Habari Mseto

Changamoto tele za makamishna wateule NLC

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MAGDALENE WANJA na OUMA WANZALA

TUME ya Kitaifa ya Ardhi ( NLC) bado inakabiliwa na changamoto tele katika hatua yake ya kuwapata makamishna wapya.

Siku chache baada ya mahakama kusimamisha kwa muda hatua ya kuwapa ofisi wateule, Taasisi ya Masoroveya wa Kenya (ISK) sasa inasema kuwa waliochaguliwa kwa nafasi hizo ‘hawakufuzu’.

Masoroveya hao walidai Ijumaa kuwa, tume hiyo imekuwa ikiwapa kazi makamishna ambao hawana ujuzi wowote kuhusu maswala ya ardhi na hivyo kusababisha matokeo duni kazini.

“Ni matarajio ya Wakenya kuwa watu wanaoteuliwa kuchukua nafasi hizo za kazi wana uzoevu na ujuzi wa maswala ya ardhi, lakini inasikitisha kwamba wengi wao hawana ujuzi wowote,” akasema Rais wa ISK Bw Abraham Samoei.

Bw Samoei alilaumu sheria ya National Land Commission Act ambayo haikutilia maanani baadhi ya vipengee vya ujuzi na uzoevu katika maswala ya ardhi.

Wanachama wa shirika la ISK wakati wa mkutano na wanahabari siku ya Ijumaa, Oktoba 4, 2019. Picha/ Magdalene Wanja

Masoroveya hao pia walitaka uteuzi wa bodi ya Udhibiti wa Maswala ya Ardhi – Land Control Boards – kufanywa haraka kwani muda wa bodi iliyoko sasa tayari umekamilika.

Baadhi ya walioteuliwa kuhudumu katika nafasi hizo ni pamoja na Bw Gershom Otachi (mwenyekiti), Bi Ms Esther Murugi, Prof James Tuitoek, Bi Gertrude Nguku, Bw Reginald Okumu, Bw Kazungu Kambi, Bi Hubbie Al-Haji na Bw Alister Mutugi.

Kambi aeleza alivyofikia PhD licha ya kupata C-

Kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), Bw Kazungu Kambi hatimaye amejitokeza kueleza alivyopata shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Baraton licha ya kutopata alama ya C+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Bw Kambi ambaye aliendeleza masomo yake ya juu na sasa anasomea shahada ya uzamifu, alisema alifanya mtihani maalumu wa watu wazima chuoni humo ndipo akaruhusiwa kujiunga nacho baada ya kupata alama ya C- katika mtihani wa KCSE.

Kulingana na Chuo cha Baraton, mtihani huo huandaliwa kwa watu wenye umri wa miaka 25 na zaidi ambao hawakupata alama za kuwawezesha kujiunga na chuo kikuu lakini wanataka kusomea shahada ya biashara na masomo mengine ya kijamii.

Naibu Msajili katika Chuo Kikuu cha Baraton, Bi Elizabeth Metto alithibitisha kwamba mtihani huo ulikuwepo miaka iliyopita lakini ukasitishwa baadaye wakati Tume ya Elimu ya Juu (CUE) ilipokomesha mitihani ya aina hiyo katika mwaka wa 2017.

Uzamili

Bw Kambi alisema kwamba alijiunga na chuo hicho katika mwaka wa 2011, akafuzu mwaka wa 2015 ambapo aliendeleza masomo ya uzamili katika chuo hicho hicho.

Alipofuzu mwaka wa 2018, alianza kusomea shahada ya uzamifu katika taaluma ya fedha katika Chuo Kikuu cha Maseno.

Wakati alipokuwa akihojiwa bungeni, wabunge watatu wa ODM kutoka eneo la Pwani walitilia shaka masomo yake lakini waziri huyo wa zamani akapeleka vyeti vyote isipokuwa cha KCSE ambacho alisema kilipotea.