Habari Mseto

Chifu awaonya vijana dhidi ya kunyemelea wake za watu

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Samuel Baya

Naibu wa Chifu wa Bamburi Bw Jeremiah Machache amewataka vijiana wa eneo hilo kukomesha tabia ya kunyemelea wake za wenyewe.

Akiwahutubia wakazi katika shule ya msingi ya Majaoni wakati wa kukagua ramani ya shamba hilo kubwa, Bw Machache aliwaonya vijana hao akisema wanajidunisha kwa tabia hiyo.

“Eneo la Bamburi hasa katika kijiji hiki cha Majaoni na Utange, kuna aina mpya ya utovu wa usalama. Kuna vijana ambao sasa wameanza kuiba mabibi za watu na kuwaficha.

Hebu tabia hii ikome mara moja kwa sababu hatutairuhusu,” akasema Bw Machache.Wakazi hao walikuwa wamejumuika katika shule hiyo kukagua ardhi zao baada ya kupatiwa hati za kumiliki ardhi mwezi uliopita.

“Tunapokabiliana na tatizo la kudorora kwa usalama katika maeneo mbalimbali ya Bamburi, tumepata habari kwamba mabibi za wenyewe sasa wameanza kutoweka na wanafichwa na vijana.

“Tafadhali waambieni vijana wenu waachane na tabia hii ya kuwaficha wake za watu. Ni hatari sana,” akaonya Bw Machache.