• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Chokoraa ashangaza hakimu kuporomosha kimombo kortini

Chokoraa ashangaza hakimu kuporomosha kimombo kortini

Na RICHARD MUNGUTI

CHOKORAA aliyeshangaza mahakama moja ya Nairobi kwa kuzugumza Kiingereza sanifu akijitetea baada ya kupatikana na hatia ya kuiba jozi mbili za viatu Jumanne alihukumiwa kifungo cha miezi minne kufanya kazi katika kituo cha polisi cha Central Nairobi.

Susan Wanjiru Njoroge, mwenye umri wa miaka 40 atakamilisha kifungo hicho mnamo Machi 2021.

Wanjru alimrai hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku “amhurumie kama vile mama humhurumia mwanawe ama bintiye akikosa.”

Alijitetea kuwa sio kupenda kwake kujiingiza katika visa vya utovu wa nidhamu mbali ni shida inayompepeta.

“Sikuwa na budi ila kufanya niwezalo nipate chakula. Niliingia katika afisi ya Bw Phoustine Makokha nikachomoka na jozi mbili za viatu nilivyouza nikapata fedha za kununua chakula na kujikimu maisha,” alimweleza hakimu kwa kiingereza sanifu.

Wanjiru aliendelea kujitetea,” Maisha ya kulala kwenye barabara siyo rahisi. Uchochole umenisonga lakini nimeghairi matendo yangu. Sitarudi kuiba tena. Heri nifanye kazi ile tu nitakayopata nipate lishe.”

Wanjiru alidodokwa na machozi na kuvuta kamasi ikabidi hakimu amtulize.

Wanjiru aliomba korti imwonee huruma na kuamuru atumikie kifungo cha nje.

Alisema tangu atiwe nguvuni na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central amekuwa akifanya kazi ya kuosha sakafu na vyoo katika stesheni hiyo.

Akizugumza kiingereza kwa madaha, Wanjiru, alieleza mahakama kwamba ulimwengu umemfunza mambo mengi maovu lakini ameamua kubadilika kuwa mwema.

“Ni maadili memaa ya ubinadamu yanayompa mmoja utu na mwelekeo maishani,” Wanjiru alizugumza kwa weledi.

Wanjiru aliyeungama kwamba makazi yake rasmi ni barabara ya Koinange, Nairobi alisema akipewa adhabu ya kuwa akifanyakazi ya jamii katika kituo hicho cha polisi atafurahi kwa vile amepata kibali machoni pa walinda usalama na “utumishi kwa wote.”

“Tangu uliposhikwa umekuwa ukizuiliwa wapi,” Bi Mutuku alimwuliza mshtakiwa.

Hakimu aliamuru atumikie kifungo cha nje miezi minne na kwamba atakuwa anafanyakazi katika kituo cha polisi cha Central.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Joachim Loew aponea shoka katika timu ya taifa ya...

Watermelon mpya?