Chungeni msilipukiwe na gesi, Kuria aonya polisi Kiandutu
NA MWANGI MUIRURI
WAZIRI wa Utendakazi wa Umma Moses Kuria amedai kwamba kuna kiwanda haramu cha gesi katika Kaunti ya Kiambu kinachohudumu karibu na kituo cha polisi.
Amedai kwamba kiwanda hicho alichosema kiko katika mtaa wa Kiandutu, kiko katika hatari ya kulipuka kwa wakati wowote na walio katika hatari kuu, ni maafisa wa polisi walio na afisi zao hapo karibu.
Aliongeza kwamba kituo hicho cha gesi hakina usajili wowote wa kisheria na kwamba ni haramu, ni hatari na hivyo kinafaa kuhalalishwa au kufungwa.
Soma Pia: Embakasi: Nema yatimua maafisa wanne kwa kutoa leseni tata
Wenyeji katika mtaa huo wa viunga vya mji wa Thika waliambia Taifa Leo kwamba kiwanda hicho huambatana na ukora mwingi sana hata wa kushambuliana kwa bunduki.
“Ni kiwanda cha kipekee. Mara kwa mara huwa kunazuka vita vya ufyatuliamaji risasi katika barabara ya kuingia na kutoka kiwandani humo,” akasema jirani wa kiwanda hicho.
Hayo yanajiri huku Rais William Ruto akitoa msimamo mkali dhidi ya mamlaka za kutoa leseni kwamba wote watakaonaswa katika mtandao wa ufisadi, utepetevu na uzembe unaohatarisha maisha ya watu, watakamatwa, wafutwe kazi na kutupwa jela.
Hii ni baada ya kiwanda katika mtaa wa Embakasi kulipuka na kusababisha vifo vya watu watatu huku zaidi ya 300 wakipata majeraha.