CORONA: Baa zote kufungwa
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Wauza Vileo Nchini (ABAK) kimetangaza kuwa kiko tayari kusalimu amri endapo serikali itaamuru kwamba vilabu vyote vya usiku vifungwe kutokana na kero la virusi vya corona.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mwenyekiti wa chama hicho Gordon Mutungi alisema wataunga mkono hatua kama hiyo kwa sababu janga hilo lina madhara makubwa kuliko kampuni au sekta yoyote.
“Kile tunafanya ni kuwajibika kama sekta ya uuzaji vileo katika kuwalinda wateja wetu katika mikahawa, baa, vilabu na maeneo mengine ya burudani,” Mutungi akasema.
“Na kwa sababu serikali haijatangaza kusitishwa kwa shughuli kote nchini, tunazionyesha serikali za kaunti dhidi ya kutoa maagizo kiholela kinyume na yale yanayotolewa na Kamati ya Kitaifa ya Kushughulikia Janga hili, kwani hatua hiyo inaweza kusababisha wasiwasi,” akaeleza.
Chama hicho kilisema kimefurahishwa na hatua ya haraka na mikakati ambayo serikali ya kitaifa imechukua kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo. ikiwemo jumbe zinazotumwa na idara ya afya ya umma.
“Zaidi ya hayo ABAK pia inafurahishwa na hatua zilizowekwa na matawi ya chama chetu na wamiliki wa biashara za vile katika jitihada za kulinda maisha ya Wakenya. Hatua hizo ni kama vile kuweka mitambo ya kusafisha mikono katika baa na mikahawa,” Mutungi akasema.
Taarifa hiyo inajiri saa chache baada ya serikali ya kaunti ya Mombasa kuzima biashara zote vilabu vya usiku kwa muda wa siku 30 zijazo, kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.
Marufuku hiyo ilitangazwa na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pamoja na Kamishna wa Kaunti hiyo Gilbert Kitiyo Jumamosi, siku mbili baada ya kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kugunduliwa nchini Kenya.
Hata hivyo, Jumapili Chama cha Wamiliki wa Baa na Vilabu vya Burudani Nchini (PERAK), tawi la Mombasa lilisema kuwa hawakushauriwa kabla ya uamuzi huo kutolewa.
ABAK ilisema tayari imechapisha karatasi zenye jumbe za kutoa uhamasisho kuhusu njia za kujikinga dhidi ya virusi vya corona.
“Tutachapisha zaidi ya mabango 500,000 zenye jumbe kuhusu ugonjwa huu hatari,” Bw Mutungi akaeleza.
Chama hicho kimeonya wanachama wake na wateja wao dhidi ya kusambaza taarifa za kupotosha kuhusu maradhi hayo, maarufu kama COVID-19 ambazo zinaweza kusababisha wasiwasi.