Habari MsetoSiasa

CORONA: Bunge kufanya kikao maalum kupitisha bajeti ya ziada

April 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa litafanya kikao maalum mnamo Jumatano wiki ijayo kupitisha mswada wa kufanikisha mpango wa serikali wa kupunguza athari za mkurupuko wa virusi vya corona kwa wananchi na uchumi kwa ujumla.

Kwenye ombi alilowasilisha kwa Spika Justin Muturi, kiongozi wa wengi Aden Duale anasema wabunge pia watajadili na kupitisha bajeti ya ziada na kanuni za kufanikisha utendakazi wa Hazina ya Dharura ya kukabilia na makali ya ugonjwa wa Covid-19.

Hazina hiyo ilibuniwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumatatu wiki hii. Aliteua bodi ya wanachama 10 watakaoisimamia chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya kutengeneza pombe, Kenya Breweries Ltd Jane Karuku,

Wabunge wanatarajiwa kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru, 2020 ambao utatekeleza miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa na  Rais Uhuru Kenyatta wiki jana kama vile kufutuliwa mbali kwa aina zote za ushuru kwa wafanyakazi wanaopokea mshahara usiozidi Sh24,000 kwa mwezi.

“Katika kikao hicho ambacho kitafanyika Aprili 8 kuanzia saa nne asubuhi, wabunge watajadili mswada na kanuni zinazohusiana na hatua zilizochukuliwa kushughulikia janga la Covid-19”.

“Mswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Ushuru (Tax Law (Amendment) Bill, 2020) na utajadiliwa na kupitishwa haraka sawa na kanuni za hazina maalum ya kushughulikia athari za ugonjwa huu hatari,” akaeleza Duale, ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini, katika barua yake.

Bw Muturi aliidhinisha ombi la  Bw Duale Jumanne jioni, kwani linafungamana na sheria za bunge ibara ya 49.

Mswada huo wa marekebisho ya sheria za ushuru ulitayarishwa na Hazina ya Kitaifa kufuatia agizo la Rais Kenyatta wiki jana.

Kwenye hotuba yake kwa Taifa Jumatano wiki jana, Rais  pia alitangaza kupunguzwa kwa Ushuru Mapato (P.A.Y.E)  kwa waajiriwa ambao hupokea mshahara wa  zaidi ya Sh24,000  kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 huku ushuru wa unaotozwa faida za kampuni pia ukipunguzwa kwa kiwango hicho.

Aidha, kiongozi wa taifa alitangaza kupunguzwa kwa Ushuru wa  Ziada ya Thamani (VAT) kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14, kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha.

“Mikakati hii inalenga kuwapunguzia Wakenya mzigo wa hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na kuzuka kwa janga hili la virusi vya corona,” akaeleza Rais Kenyatta.

Bajeti ya ziada ambayo wabunge watajadili inalenga kutenga fedha kwa mpango wa kupunguza makali ya Codid-19. Waziri wa Fedha Ukur Yatani anatarajiwa kupunguza mgao wa fedha kwenye baadhi ya wizara na idara za serikali ili kutengeza fedha zaidi kwa Wizara ya Afya.

Fedha hizo zitatumiza kuajiri wahudumu zaidi wa afya, alivyoamuru Rais Kenyatta wiki jana, pamoja na kununua vifaa hitajika katika vita dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Jumanne, maseneta walirejelea vikao ambapo janga la Covid-19 lilijadiliwa kwa kina.