CORONA: Hasara kwa wakuzaji maua
Na ONYANGO K’ONYANGO
WAKULIMA wameanza kuhisi makali ya virusi vya corona baada ya kukosa kusafirisha mazao yao nje ya nchi huku mataifa mbalimbali yakiendelea kupiga marufuku safari za ndege kuzuia kusambaa kwa maradhi hayo.
Wakulima sasa wanahofia kuwa huenda wakapata hasara kubwa kwa kukosa soko.
Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Micah Cheserem anayemiliki kampuni ya maua ya Equator Flowers ambaye pia ni mkuzaji wa parachichi mjini Eldoret, alisema kuwa ameshindwa kupeleka maua yake barani Ulaya.
“Baada ya China, bara la Ulaya sasa limegeuka kuwa kitovu cha maradhi ya virusi vya corona. Asilimia 90 ya maua yetu tunauza Ulaya. Kusitishwa kwa safari za ndege ni pigo kubwa kwetu,” akasema Bw Cheserem.
“Soko la maua limefungwa, hakuna wanunuzi. Kwa mfano, kampuni ya Equator Flowers tulitupa tani 12 za maua baada ya mawakala wetu wa nchini Uswisi kutufahamisha kukoma kuwatumia maua,” akasema Meneja Mkuu wa Equator Flowers, Bw Nehemiah Kangogo.
Kulingana na taarifa zilizochapishwa katika tovuti ya kampuni ya Royal FloraHolland ambayo huusika na uuazaji wa maua nchini Uswisi, asilimia 20 ya maua yameharibiwa katika kipindi cha wiki chache zilizopita kutokana na ukosefu wa wanunuzi.