Habari Mseto

'Corona ipo, sio mzaha'

April 22nd, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

“UGONJWA wa virusi vya corona upo! Unatesa na si wa kuchezewa. Nimepitia magumu tangu nilipoambukizwa. Ni maradhi hatari. Nawaomba Wakenya wajichunge. Huu sio mchezo!”

Hii ni kauli ya Bi Faith Gaci (pichani), aliye na miaka 28, baada ya kuruhusiwa kuondoka katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta jijini Nairobi mnamo Jumatatu wiki hii, alipothibitishwa kupona virusi vya corona.

Faith anawahimiza Wakenya kujichunga na kufuata taratibu na kanuni zilizotolewa na serikali kuzuia maambukizi ikiwemo kuepuka maeneo yenye watu wengi, kunawa mikono mara kwa mara na kuvaa maski.

“Niliyoshuhudia mwenyewe ni magumu na mazito. Covid-19 ni hatari. Watu wajichunge sana sana,” Faith aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano jana.

Kufikia jana watu 296 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hapa nchini tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa mwezi uliopita.

Ugonjwa huo uliozuka nchini China mwishoni mwa mwaka jana hauna dawa wala chanjo.

Faith, ambaye ni mfanyabiashara wa kuuza dawa jijini Nairobi, alikuwa ametengwa hospitalini kwa muda wa siku 31 pamoja na wagonjwa wengine wakipokea matibabu.

Alisema aliambukizwa virusi vya corona na mmoja wa wafanyakazi wake.

“Nina duka la kuuza dawa mtaani Buruburu jijini Nairobi. Mume wa mfanyikazi wangu aliambukizwa alipoenda ng’ambo na aliporudi akaambukiza mkewe ambaye naye alinisambazia,” Faith akaelezea, akiongeza kwamba mfanyakazi huyo hakuwa na dalili zozote za kuugua.

Anasema dalili za mwanzo alizopata ni kuhisi mafua, kufungana mapua na matatizo ya kupumua. Baadaye kiwango chake cha joto kilipanda, akaanza kuumwa na kichwa na kupata kikohozi kizito ndiposa akaamua kwenda hospitalini.

“Nilienda hospitali moja mtaani, na baada ya kufanyiwa ukaguzi nikaonekana kuwa na dalili za Covid-19. Walichukua sampuli na baada ya uchunguzi ikathibitishwa ninaugua,” akasimulia msichana huyo ambaye kwa sasa anasema ametulia nyumbani kwao Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

“Ilipothibitishwa ninaugua nilitengwa mara moja pamoja na mfanyakazi wangu aliyeniambukiza na mumewe, na tukapelekwa katika hospitali ya Chuo cha KU tulikokuwa tunapata matibabu yaliyojumuisha tembe na sindano,” akaelezea.

Alieleza kwamba wagonjwa pia wanaongezwa mji mwilini mara kwa mara.

Wizara ya Afya imesema ugonjwa huo unatibiwa kwa dawa za kukabiana na dalili kama vile joto, homa na kusaidia kupumua.

Wataalamu wanaeleza uwezo wa mtu kupona maradhi hayo unategemea kinga yake ya magonjwa.

Hospitalini KU, Faith asema aliwekwa katika chumba ambapo walikuwa jumla ya wagonjwa watano, vyoo na bafu wakitumia kwa pamoja.

“Umbali baina ya mtu na mwenzake unatiliwa maanani kwenye chumba cha wagonjwa,” akaeleza.

Alisema madaktari hukagua wagonjwa asubuhi na jioni na wauguzi wakijukumika kuwatazama mara kwa mara.

Alifichua kwamba ilimgharimu Sh25,000 kupata matibabu.

Anawahimiza Wakenya kukoma kuwachukulia kwa ubaya watu wanaougua ugonjwa huo akisema kwa sasa analazimika kukaa nyumbani kwao kutokana na kuwa watu wanamchukua kuwa hatari na anayeweza kuwasambazia virusi hivyo licha ya kuwa amepona.

Wakati huo huo, dereva aliyewekwa karantini kwa kusafirisha waombolezaji kwa mazishi katika Kaunti ya Homa Bay amesema hajapewa dawa zozote tangu alipotengwa siku tano zilizopita.