CORONA: Kenya yafunga mpaka wake na Uganda
Na Gaitano Pessa
MAAFISA katika mpaka baina ya Kenya na Uganda katika Kaunti ya Busia wamefunga Kituo Kikuu cha Mpaka Busia (OSBP) na kupunguza safari za watu kati ya Kenya na Uganda.
Hii ni katika juhudi zinazolenga kuimarisha mikakati ya serikali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Hatua hiyo imejiri siku moja tu baada ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuamrisha kufungwa kwa mipaka yake, saa chache tu baada ya nchi hiyo kutangaza kisa chake cha kwanza cha Covid-19.
Akitoa taarifa jana kutoka Busia OSBP, Kamishna wa Kaunti Joseph Kanyiri, alisema kufungwa kwa vituo hivyo ni kwa maslahi ya raia wa mataifa hayo mawili.
“Mpaka huo umefungwa kwa matumizi ya binadamu kumaanisha kwamba hakuna atakayeingia kutoka Uganda au kutoka Kenya. Tunawahimiza walio na mipango ya kusafiri Uganda kufutilia mbali safari zao ili wasije wakakwama Busia,” akasema.Mabasi pia yamesitisha safari.
Alisisitiza kwamba mabasi yote yanayofanya kazi baina ya miji mingine na Busia yanapaswa kuratibu upya ratiba zao kwa abiria ambao walikuwa wamelipia safari hadi maagizo mengine yatakapotolewa kuambatana na maagizo ya serikali.
“Kumekuwa na tangazo kutoka kwa serikali zote za Kenya kwamba hazitaruhusu raia kutoka mataifa yaliyoripotiwa kuwa na Covid-19 ikiwemo Uganda.”
Kwa sasa, kupitia majadiliano na kamati za usimamizi wa mipaka katika vituo vya Busia na Malaba, trela zinazosafirisha mizigo katika pande husika zitaruhusiwa kuingia lakini zikiwa na wahudumu wawili pekee.