• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
CORONA: KICD kutoa mafunzo redioni

CORONA: KICD kutoa mafunzo redioni

Na FAITH NYAMAI

WIZARA ya Elimu imewashauri wazazi kuwaruhusu watoto wao kufuatilia matangazo ya elimu yanayotolewa na Taasisi ya Kukuza Mitaala Kenya (KICD), baada ya shule kufungwa kutokana na tisho la virusi vya corona.

Waziri wa Elimu George Magoha, Jumatno aliwashauri wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wako salama na wanakaa nyumbani ili waweze kufuatilia masomo.

KICD imebuni ratiba ambayo itahakikisha kuwa wanafunzi wote katika kiwango cha shule za msingi na upili wamefaidika.

Taasisi hiyo imeshirikiana na Shirika la habai la KBC kutoa matangazo hayo kupitia vipindi vya redio.

Masomo hayo yatatangazwa kutoka Jumatatu hadi Ijumaa kupitia KBC Radio Taifa na KBC Idhaa ya Kiingereza.

Waziri alisema kuwa vipindi vya Radio Taifa vitakuwa vikipeperushwa kutoka saa nne hadi saa tano mchana, huku vipindi vya idhaa ya Kiingereza vikipeperushwa kutoka saa tatu na robo asubuhi hadi saa sita adhuhuri na saa nane hadi saa kumi alasiri.

“Vipindi hivyo pia vitatangazwa kupitia idhaa za redio za Iftini FM na Transworld Radio katika kaunti za Garissa, Mandera na Wajir,” akasema Prof Magoha.

Kituo cha televisheni cha Edu, ambacho kinamilikiwa na KICD pia kitakuwa kikitoa matangazo hayo kila siku na pia kupitia mtandao wa YouTube.

Kulingana na ratiba ya masomo mwaka huu, shule za msingi na upili zilitarajiwa kufungwa Aprili 10.

Mnamo Jumapili, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza shule zote kufungwa mara moja.

Taasisi za elimu ya juu kama vyuo vikuu nazo ziliamriwa kufungwa kufikia kesho.

Hatua hiyo inalenga kupunguza maambukizi ya virusi hivyo nchini.

You can share this post!

Tafadhali msisafiri mashambani, wakazi wa mijini waombwa

Magelo aitisha kikao kuokoa soka nchini

adminleo