CORONA: Madaktari wadai makao maalumu
Na BENSON MATHEKA
MADAKTARI na wahudumu wa afya nchini wanataka serikali iwape makao maalumu ili waishi mbali na familia zao wakisema wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa virusi vya corona wakiwa kazini na kusambaza nyumbani kwao.
Kulingana na kaimu katibu mkuu wa chama cha madaktari na wataalamu wa meno (KMPDU), Dkt Chibanzi Mwachonda, kwa kushughulikia wagonjwa na kurudi nyumbani, madaktari wanahatarisha maisha ya familia zao.
“Madaktari wanahitaji kupatiwa makao kwa sababu wanahudumu katika mazingira hatari sana na wanahitaji kukinga familia zao,” alisema Dkt Chibanzi Mwachonda.
Alisisitiza kuwa madaktari na wahudumu wa afya wanahitaji vifaa vya kutosha vya kujikinga ili wasiambukizwe corona wanapowashughulikia wagonjwa.
“Mbali na kuhitaji vifaa vya kutosha vya kujikinga, madaktari na wahudumu wa afya kwa jumula wanahitaji kutengwa na familia zao kwa kupatiwa makao maalumu. Tumeona hilo likifanyika katika mataifa mengine kama Italia ambako wahudumu wengi wa afya wameambukizwa virusi hivi wakiwa kazini,” alisema Dkt Chibanzi kwenye mahojiano.
Wahudumu wa afya zaidi ya 50 wamekufa Italia baada ya kuambukizwa corona.
Dkt Chibanzi alisema kwamba njia ya pekee ya kuhakikisha madaktari wanaoambukizwa wamekinga familia zao ni kuwapa makao maalumu kama vile kuwahifadhi katika hoteli.Kulingana na katibu huyo, wahudumu wa afya pia wanahitaji ushauri nasaha kutokana na wanayopitia wakishughulikia janga hili.
Alisema corona ni janga linaloshuhudiwa ulimwenguni kwa mara ya kwanza na wahudumu wa afya wanafaa kuandaliwa kisaikolojia kabla na baada kuwahudumia wagonjwa.
Akihojiwa na runinga ya Citizen Jumatatu asubuhi, katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini (KRC) Dkt Asha Mohammed, alisema shirika hilo liko tayari kuwasaidia wahudumu wa afya kwa kuwapa ushauri nasaha.
Alisema madaktari wanapaswa kulindwa kwa hali na mali wakati huu ambao wamejitolea kukabiliana na janga hili linalozua hofu kote ulimwenguni.
Waziri wa afya Mutahi Kagwe amekuwa akisisitiza kuwa serikali itawasaidia wahudumu wa afya kwa kazi muhimu wanayotekeleza wakati huu visa vya maambukizi ya virusi vya corona vinavyoongezeka nchini.
Alisema hayo huku wataalamu wa afya wakitilia shaka uwezo wa Kenya kukabiliana na maambukizi ya virusi hivi yakiongezeka inavyofanyika katika mataifa mengine.
Baadhi ya wataalamu wanasema Kenya haina madaktari na vifaa vya kutosha kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.