Habari Mseto

CORONA: Samburu yapiga marufuku biashara ya miraa

March 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Kaunti ya Samburu imepiga marufuku usambazaji na uuzaji wa zao la miraa kwa wiki mbili katika juhudi zanazolenga kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya corona.

Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kikamilifu kuanzia Machi 20 na huenda wafanyibiashara katika sekta hiyo wakaandikisha hasara wakati marufuko hayo yakitekelezwa.

Kaunti hiyo pia imewashauri wafanyibiashara katika masoko ya kuuza mifugo kujizuia kutangamana kwenye vikundi vya watu zaidi ya 15.

Wakati huo huo viongozi wakuu katika serikali ya kaunti ya Samburu wamepanga kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti ya dharura ili kusaidia kuwapa mafunzo manesi kukabiliana na virusi hivyo vya Corona.

Pia, idara ya afya imetenga wadi spesheli katika vituo vitatu vya afya kwa kila kaunti ndogo ili kuwashughulikia waathiriwa wa virusi vya Corona iwapo vitazambaa Samburu.

Naibu gavana wa Kaunti hiyo Bw Julius Leseeto amesema kuwa wamebuni kamati itakayosaidia kupasha umma habari kuhusiana na hali ya virusi hivyo.

“Tayari tumetenga wadi kadhaa kwa kila kituo cha afya kwenye kaunti yetu. Tutaongeza vyumba vingine iwapo kutakuwa na hitaji la kufanya hivyo,” alisema Naibu gavana.

Aliongeza: “Kwa sasa manesi wote wamefunzwa namna ya kuwashughulikia waathiriwa wa virusi vya Corona. Vituo vya afya ambavyo vimepokea vitanda maalum ni Maralal, Wamba na Baragoi,” alisema Bw Leseeto.

Wakati huo huo, Waziri wa afya katika kaunti ya Samburu Bw Stephen Lekupe ametoa wito kwa wakazi kufuata masharti yaliyowekwa ili kuepuka kupata virusi vya Corona.

Sheria hizo ni pamoja na kutosalimiana kwa kwa mikono, kunawa mikono kila wakati kutumia viyeyushi na kukumbatiana.

Alihimiza wale watakaonesha dalili za virusi hivyo wajisalimishe kwenye vituo vya afya vilivyo karibu.