Habari Mseto

CORONA: Visa vyafika 81, wawili wapona

April 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA FAUSTINE NGILA

SERIKALI imethibitisha visa vingine 22 vya virusi vya corona Jumatano, huku idadi kamili ikifika visa 81.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kati ya watu hao 22, 18 ni Wakenya, wawili ni raia wa Cameroon na wawili raia wa Pakistan.

Aidha alitangaza kuwa wagonjwa wawili wa virusi hivyo wamepona baada ya siku 23 za kujitenga.

“Leo tuna habari njema kwa kuwa mgonjwa wa kwanza wa corona nchini Brenda Cherotich amepona. Brian Orinda pia amethibitishwa hana virusi hivyo baada ya kupimwa mara mbili,” akasema waziri huyo.

Pia, alifafanua kuwa maori ya kusafirisha chakula yataruhusiwa barabarani wakati wa kafyu, na kwamba polisi wamejulishwa kuhusu suala hilo.

Alizitaka kampuni za maji zisiwakatie wakazi wa mijini maji huku akiomba malandilodi kukoma kuwakatia wapangaji stima.

“Mtu yeyote asikatiwe maji wala stima. Tunaishi katika hali ngumu,” akasema.

Kuhusu iwapo Kenya ina mpango wa kutekeleza hali ya kubana watu kwa nyumba zao bila kutoka nje, Bw Kagwe alisema uamuzi kama huo unaweza kuchukuliwa lakini kwa umakini sana.

“Hebu fikiria watu kumi wamefungiwa kwa chumba kimoja na mmoja wao amebeba virusi hivyo ila hajui. Hapo atawaambukiza watu wote, hali inayohatarisha maisha ya watu hata zaidi. ‘Lockdown’ haifai kukimbiliwa isipokuwa wakati hatuna namna nyingine ya kupunguza maambukizi, lakini lazima ifanywe kwa utaratibu,” alisema.