CORONA: Wanaosafiri kwa kaunti mpya kupimwa
Na WAANDISHI WETU
BAADHI za kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa zimeanzisha vituo vya kupima wasafiri wanaoingia kwenye kaunti hizo, lengo kuu likiwa kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.
Vituo hivyo vimeanzishwa katika maeneo ya mipaka ya kaunti hizo na nyingine japo baadhi ya wasafiri wanaonekana kukerwa na shughuli hiyo.
Hata hivyo, maafisa wa kaunti hizo kama Turkana na Elgeyo Marakwet wamesema hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha virusi hivyo ambavyo vimeangamiza maisha ya watu wanne nchini havifiki kwenye kaunti hizo.
Katika Kaunti ya Turkana, wasafiri wanaotumia ndege na magari wamekuwa wakipimwa katika maeneo ya kuingia kwenye gatuzi hilo kubaini iwapo wana virusi hivyo au la.
Kwa mujibu wa Mkurgenzi wa Huduma za matibabu wa gatuzi la Turkana Dkt Gilchrist Lokoel, zaidi ya wasafiri 70,000 wamepimwa virusi vya corona. Abiria hao walipimwa katika vituo vya Kainuk, mpaka wa Nadapal, Lokichoggio, Lodwar na viwanja vidogo vya ndege vya Kakuma na Kapese.
Kufikia Jumatano asubuhi, Dkt Lokoel alisema watu 72,401 walikuwa wamepimwa na wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika magatuzi yote madogo ya kaunti ya Turkana.
Wale ambao wamekuwa wakisafiri kutoka Kitale hadi Lodwar, wamekuwa wakipimwa Kainuk, Lokichar na karibu na Chuo Kikuu cha Turkana.
Dkt Lokoel aliwataka wasafiri na wakazi washirikiane na wahudumu wa afya wanaotekeleza vipimo hivyo ili wawe na uhakika kwamba hawana virusi hivyo.
Katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, serikali ya Gavana Alex Tolgos, imekuwa ikiwapima watu wanaoingia na kutoka gatuzi hilo kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona.
Wahudumu wa afya wa kaunti hiyo jana walianza kuwapima watu kwenye mpaka wa kaunti hiyo na ile ya Uasin Gishu kwenye barabara ya Iten-Eldoret ambao zaidi ya abiria 2,000 walipimwa.
“Tunawapima kiwango cha joto mwilini na iwapo kuna kisa chochote kinachoshukiwa, sisi hushirikiana na madaktari kukishughulikia,” akasema Waziri wa Afya wa Elgeyo Marakwet Kiprono Chepkok.
“Abiria wanaoshukiwa watatengwa. Tunafanya haya ili kuwalinda watu wetu,” akaongeza.
Wakati huo huo, watu saba ambao walikuwa wametengwa kwa kushukiwa kuwa na virusi vya corona jana waliruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kukosa kupatikana na virusi hivyo.
Naibu Gavana wa Elgeyo Marakwet Wesley Rotoch naye alisema abiria watakuwa wakipimwa katika vituo vya Kapcherop, Kipsaos, Liter na Cheploch.
“Tungependa kuwashukuru wananchi kwa kushirikiana na wahudumu wa afya wakati wa kushiriki vipimo vya virusi hivyo. Tunawashauri waendelee kuzingatia viwango vya juu vya usafi,” akasema Bw Rotich.
Wakati huo Muungano wa Kiuchumi wa Magavana wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, umetoa wito kwa serikali kuu itoe barakoa na mavazi ya kuwasaidia raia kujikinga na viini vya corona.
Kwenye taarifa yao ya pamoja iliyosomwa na Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago, muungano huo ulitoa wito kwa serikali kusambaza mavazi hayo na pia kuwataka wakazi wanaoishi mijini kutorejea mashambani hadi janga la sasa liishe.
Ripoti za Evans Kipkura, Onyango K’onyango na Sammy Lutta