• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Corona yageuza mazingira ya usomaji bajeti bungeni

Corona yageuza mazingira ya usomaji bajeti bungeni

Na CHARLES WASONGA

BAJETI ya mwaka wa kifedha 2020/21 ilisomwa Alhamisi, Juni 11, 2020, katika mazingira ya kipekee bungeni kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili kutokana na masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo wabunge huhudhuria shughuli hiyo kwa wingi, ni wabunge 66 walioruhusiwa ukumbini kusikiliza hutoba ya Waziri wa Fedha Ukur Yatani.

Hii ni kulingana na mwongozo uliotolewa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi unaolenga kuzuia msongamano wa wabunge ukumbini, kuafiki masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya.

Wengine waliosalia walilazimika kufuatilia hotuba ya waziri kupitia runinga zilizowekwa katika vyumba maalum katika majengo ya bunge ikiwa ni pamoja na eneo na maakuli. Na baadhi yao pia walifuatilia hotuba hiyo katika afisi zao.

Kando na miaka ya nyuma ambapo Waziri wa Fedha alikuwa akiwasili katika majengo ya bunge akiandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa wizara yake, Alhamisi Balozi Yatani, aliandamana na maafisa 30 pekee.

Miongoni mwao alikuwa Waziri Msaidizi katika wizara hiyo Nelson Gaichuhie na Katibu katika Wizara hiyo Saitoti Torome.

Na alipofika katika majengo ya bunge, Bw Yatani alilakiwa na idadi ndogo zaidi ya wabunge wakiongozwa na kiongozi wa wengi Aden Duale na mwenzake wa wachache John Mbadi. Mwingine alikuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kimani Ichung’wah.

Ulinzi ulikuwa mkali ndani na nje ya majengo ya bunge huku maafisa wa usalama wakihakikisha kuwa raia na wafanyakazi wa bunge wanadumisha masharti ya kutokaribiana ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Na ni takriban wanahabari 50 pekee walipewa kibali cha kuingia ndani ya majengo ya bunge, miongoni mwao wakiwa wapigapicha za runinga na waandishi wa magazeti.

Na maafisa wa idara ya usalama bunge wakiongozwa na karani Michael Sialai walishika doria kuhakikisha kuwa wanahabari wote wamevalia barakoa na kudumisha hitaji la kila mmoja kuwa umbali wa mita moja kutoka aliko mwenzake.

Isitoshe, tofauti na miaka ya nyuma ambapo wabunge wangepata fursa ya kuongea na wanahabari wakitoa kauli zao kuhusu bajeti, hali haikuwa hivyo.

Spika Muturi aliamuru baada ya hotuba ya Waziri Yatani “kila mtu aende zake kwa amani huku akihakikisha anatii kanuni za kuzuia maambukizi ya Covid-19.”

Vinywaji na vitafunio ambavyo huandaliwa kwa wageni wakati wa shughuli kama hiyo pia havikuwepo Alhamisi.

  • Tags

You can share this post!

Machungu ambayo Wakenya watapitia kufadhili bajeti ya mwaka...

Michezo yatengewa asilimia kubwa zaidi ya bajeti katika...

adminleo