• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Corona yasababisha mfadhaiko katika jamii

Corona yasababisha mfadhaiko katika jamii

LAWRENCE ONGARO

HOMA ya corona imesababisha masaibu mengi katika jamii, huku kukiwa na matukio mengi tofauti.

Kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Kiambu alisema uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa migogoro na dhuluma za kifamilia, utumizi wa dawa za kulevya, na unywaji holela wa pombe ni baadhi ya matukio yanayoshuhudiwa hasa wakati huu dunia inapambana na corona.

“Tumeshuhudia vifo vingi kutokana na msongo wa mawazo, na pia familia kuzozana kila mara,” alisema Bw Nuno.

Alisema wanafunzi wengi wa shule wa kike wamepachikwa mimba hasa wakati huu shule zimefungwa kufuatia corona.

“Msichana yeyote aliyedhulumiwa anastahili kupiga ripoti kituo cha polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Bw Nuno.

Jambo lingine ni kuongezeka kwa ajali za barabarani hasa pikipiki za bodaboda.

“Unapozuru vituo vingi vya polisi utapata pikipiki nyingi zilizofanya ajali. Vijana wengi wanaoendesha pikipiki hawana leseni maalum huku pia wakikosa kufuata sheria za trafiki,” alisema afisa huyo.

Alitoa mwito kwa wahudumu wa bodaboda kufuata sheria wakati wowote wakiendesha pikipiki zao.

Alisema wakati kulikuwa na vizuizi vya polisi katika maeneo tofauti hapa nchini, wahudumu wa bodaboda wengi walikiuka sheria kwa kupita njia za mkato wakiwa wamewabeba wasafiri.

“Tungetaka wananchi popote walipo wafuate sheria zilizowekwa ili wasiendelee kupingana na serikali. Polisi wanafuata sheria zilizoko na hawana ubaya wowote na mwananchi,” alisema Bw Nuno.

Alisema kituo cha polisi kiko wazi kwa mwananchi yeyote na kwa hivyo “ukidhulumiwa kwa njia yoyote ile una haki ya kwenda huko.”

  • Tags

You can share this post!

Shughuli za ujenzi wa uwanja wa kisasa Mombasa zashika kasi

AFYA: Barakoa chafu zinavyosambaza corona vijijini

adminleo