• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Coronavirus: Wafanyakazi wa serikali wapigwa marufuku kusafiri ng’ambo

Coronavirus: Wafanyakazi wa serikali wapigwa marufuku kusafiri ng’ambo

PSCU NA Waandishi Wetu

SERIKALI imepiga marufuku maafisa wake kufanya ziara nje ya nchi isipokuwa tu kwa sababu zenye umuhimu mkubwa.

Kwenye kikao kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kamati ya Kitaifa ya Dharura ya kukabiliana na virusi vya corona katika Ikulu jana, Wakenya wote wanaorejea nchini pamoja na wageni kutoka maeneo yenye hatari zaidi, wameamrishwa kujitenga kwa muda usiopungua siku 14 mfululizo.

Wafanyabiashara na wananchi pia wameshauriwa kutofanya ziara zisizo muhimu hususan katika maeneo yaliyo na hatari zaidi.

Rais pia aliagiza bajeti kufanyiwa mabadiliko katika harakati za kuchukua hatua za kuzuia na kukabiliana na virusi vya corona.

Rais Kenyatta pia aliagiza kuandaliwa kwa mikakati mwafaka ya kulinda watu wenye mapato ya chini na watu wanaokabiliwa na hatari hususan katika mitaa ya mabanda.

Juhudi hizi zitategemea mifumo iliyopo ya kijamii wakiwemo machifu, wasimamizi wa wadi, viongozi wa kidini na wazee wa nyumba kumi kueneza ufahamu na kushirikisha juhudi za kuzuia na kukabiliana na virusi hivyo.

Wakati huo huo, wahudumu katika Hospitali ya Moi, Eldoret (MTRH) mnamo Jumatano jioni waliwekwa katika hali ya tahadhari baada ya habari kuenea kwamba mfanyakazi aliyekuwa amesafiri Nigeria alikuwa na virusi vya corona.

Lakini usimamizi wa MTRH kwenye taarifa kwa vyombo vya habari ulikanusha habari hizo.

“Tunataka kuhakikishia umma kwamba hakuna mtu ambaye amepatikana na virusi vya corona hapa MTRH. Vilevile hakuna kisa kama hicho ambacho kimeripotiwa maeneo mengine ya nchi,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji Dkt Wilson Aruasa.

Dku Aruasa alieleza kuwa hospitali hiyo imetenga vitanda 10 na vingine 15 ambavyo vimefadhiliwa na Benki ya Dunia vitakuwa tayari kufikia Jumapili hii.

Kaunti ya Uasin Gishu ni kati ya zile ambazo zimetajwa kuwa kwenye hatari ya kukumbwa na visa vya maambukizi ya corona.

Hospitali hiyo ya MTRH inashirikiana na usimamizi wa uwanja wa ndege wa Eldoret kuwakagua abiria wanaoingia nchini kutoka nchi za kigeni, ili kuzuia watu walio na ugonjwa huo kuusambaza nchini.

Wakati huo huo, Seneta wa Uasin Gishu Prof Margaret Kamar ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) kutenga vyumba maalum vya kuwafungia abiria wanaoshukuwa kuwa na virusi vya corona kwa siku 14 katika viwanja vyote nchini.

Prof Kamar alikashifu serikali kwa madai ya kutochukulia kwa uzito virusi vya corona.

“Tuna wasiwasi kuhusu namna ambavyo serikali imekuwa ikishughulikia virusi vya corona. Tunafaa tuwe na maeneo ya kuwatenga raia katika viwanja vyote vya ndege nchini,” akasema Prof Kamar.

You can share this post!

Korti yatupa kesi ya uchochezi dhidi ya Kuria

Wakuu serikalini walaumiwa kwa mauaji nchini

adminleo