Habari Mseto

Covid-19: Sababu za Rais kudinda kulegeza kamba

June 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Katika hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumamosi na iliyotarajiwa na Wakenya ingekuwa yenye afueni masharti yaliyowekwa kudhibiti msambao wa Covid – 19 yangelegezwa wakiyataja “yamechangia maisha kuwa magumu”, ni bayana Kenya haijajiandaa kikamilifu kukabiliana na janga hili.

Katika utangulizi wa hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu, Nairobi, kupitia runinga, Rais Kenyatta alieleza manufaa na hatari inayoweza kuibuka ikiwa masharti yatalegezwa.

Alisema iwapo mikakati na masharti yanayoendelea kutekelezwa hayangewekwa, kufikia Julai 1, 2020, Kenya ingekuwa na zaidi ya maambukizi 800, 000 ya virusi vya corona, kwa mujibu wa mukhtadha wa mataifa yaliyoathirika pakubwa kwa kupuuza ushauri wa Shirika la Afya Duniani.

Endapo serikali haingekaza kamba masharti, alionya kuwa kufikia mwezi Julai 2020, taifa hili lingekuwa na maafa zaidi ya 74, 000. “Leo hii tukilegeza kwa asilimia 20 mikakati na masharti tuliyoweka, maambukizi yatapanda hadi wagonjwa 200, 000 na maafa 30, 000,” Rais Kenyatta akaeleza.

Ni kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi kila uchao, Rais Kenyatta amesema masharti yaliyowekwa, hasa kafyu ya kitaifa na amri ya kutoingia na kutotoka kaunti ya Nairobi, hayatalegezwa.

Badala yake, kafyu ya kila siku inayoanza saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi, saa hizo zimetathminiwa na kuwa kati ya saa tatu hadi saa kumi asubuhi, kuanzia Jumapili, Juni 7, 2020. “Tathmini hii ya saa itawezesha Wakenya kurejelea ratiba ya kila siku kufanya kazi,” kiongozi wa nchi akasema.

Kafyu ya kitaifa na iliyoanza kutekelezwa Machi 27, 2020 itaendelea kwa muda wa siku 30 zaidi, kutoka Juni 6.

Hotuba ya Rais Kenyatta ilikuwa yenye afueni kwa wakazi wa mtaa wa Eastleigh – Nairobi na Mji wa Kale – Mombasa kufuatia amri ya kutoingia na kutotoka mitaa hiyo kuondolewa kuanzia Jumapili, Juni 7. Kaunti ya Kwale na Kilifi, amri hiyo imeondolewa.

Aidha, kufuatia ongezeko la maambukizi Nairobi na Mombasa, amri ya kutoingia na kutotoka, itaendelea kwa muda wa kipindi cha siku 30 zaidi, Rais Kenyatta akisema kufungua kaunti hizo itakuwa sawa na “kutengeneza jukwaa la msambao wa Covid – 19 katika maeneo mengine nchini”.

Hata hivyo, kitovu cha hotuba ya Rais kilionekana kuegemea mdahalo wa maambukizi katika kaunti, kudhibiti usambaaji wa virusi vya corona. Rais alisema kaunti zilizoathirika ili kuruhusiwa kufunguliwa, sharti zionyeshe ukakamavu wake katika mikakati iliyowekwa kuzuia maambukizi.

Akitoa mfano wa kaunti ya Siaya na Busia, kama miongoni mwa zisizo na vituo vya afya vyenye idadi ya kutosha ya vitanda, Rais Kenyatta alisema kila kaunti inapaswa kuwa na kituo chenye zaidi ya vitanda 300 kulaza wagonjwa wa Covid – 19 ili uchumi ufunguliwe kikamilifu.

Aidha, alisema mnamo Jumatano, Juni 10, 2020, atafanya mkutano na magavana wote 47, chini ya Baraza la Magavana nchini, CoG, ili kujadili maandalizi ya kila kaunti. “Nimeita mkutano wa Baraza la Gavana nchini Jumatano, ili tuongee na magavana wote vile tutaruhusu watu kutembea,” Rais akasema.

“Serikali zote za kaunti lazima ziweke mikakati kupima wanaoingia. Tuhakikishe hatutoi ugonjwa kutoka kaunti moja hadi nyingine,” kiongozi wa taifa akaeleza.

Katika kipindi hiki, serikali za kaunti zimetengewa kima cha Sh5 bilioni kushughulikia Covid – 19.

Awali, wizara ya afya ilitangaza kuwa vituo vya afya nchini vimejaa na kwamba vimeanza kulemewa na idadi ya juu ya maambukizi. Waziri katika Wizara husika Mutahi Kagwe alisema serikali imeanza kutathmini namna watu wataweza kujitunzia wagonjwa wa Covid – 19 nyumbani.

Hata hivyo, ni suala ambalo linakanganya serikali, Rais Kenyatta akitilia shaka uwezo wa watu kuweza kutunza waathiriwa. “Ni swali gumu, Wakenya wataweza kudhibiti janga hili kwa kujichungia wagonjwa nyumbani ilhali vituo vya afya vimelemewa?” akahoji.