COVID-19: Serikali yakana madai raia wa China wanatoroka nchini Kenya
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI imekana madai kuwa raia wa China wanatoroka nchini kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Ijumaa, Julai 31, 2020, alisema raia wa China walioondoka nchini kabla ya safari za ndege za kimataifa kurejelewa Agosti 1, 2020, walikuwa wamefanya mipango ya kusafiri kwa kutumia taratibu zilizoidhinishwa.
Alisema kuondoka kwa Wachina hao ni sawa na mpango ambao Kenya ilitekeleza miezi miwili iliyopita ya kuwarejesha nyumbani raia wake waliokuwa wakiishi katika mataifa mbalimbali ya ng’ambo baada ya kuripotiwa kwa mlipuko wa Covid-19.
Mnamo Ijumaa asubuhi iliripotiwa kuwa mamia ya Wachina walipiga foleni katika uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) tayari kuabiri ndege iliyokodiwa kuondoka nchini.
Walikuwapo watoto na wanawake.
Lakini Bw Kagwe baadaye jioni akawaambia wanahabari jijini Nairobi kwamba; “Kuna raia wengi wa China humu nchini na safari zao sio jambo muhimu sasa. Kuna Wakenya wengi walioondoka mataifa mengi kwa njia hiyo hiyo kwa hivyo isionekana kana kwamba walitoroka kutokana na hofu yoyote.”
“Hakuna kile ambacho wanajua na sisi hatujui. Wanasafiri tu kama watu wengine,” akaeleza huku akipuuzilia madai kuwa Serikali ya China imeamua kuondoa raia wake Kenya kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.
Itakumbukwa kuwa mnamo mnamo Juni 2020 Serikali ya Kenya pia ilikana madai kuwa jumla ya Wachina 200 waliondoka nchini majira ya usiku kwa hofu ya janga la corona.