• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Covid-19 yaathiri huduma katika wizara kadhaa

Covid-19 yaathiri huduma katika wizara kadhaa

Na CHARLES WASONGA

VIRUSI vya corona ambavyo vinavyoendelea kuambukiza idadi kubwa ya watu nchini vimevuruga shughuli katika afisi mbalimbali za serikali kuu.

Baadhi ya wizara zilizoathirika ni; Fedha, Masuala ya Ndani, ICT, Ardhi, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ambazo sasa zimesitisha baadhi ya huduma baada ya kurekodi visa vya kadha vya maambukizi.

Mnamo Jumatatu, Julai 13, 2020, wiki hii Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Magereza Zeinab Hussein aliamuru wafanyakazi wote katika afisi za idara zilizoko jumba la Teleposta Towers waende karantini ya nyumbani kwa siku 14 baada ya mmoja wao kufariki kutokana na Covid-19.

Katika barua kwa wafanyakazi hao, Bi Hussein alisema wafanyakazi wachache wanaotekeleza huduma muhimu ndio wataruhusiwa kuendelea na kazi.

“Kwa hivyo, naamuru ni maafisa wawili pekee kutoka kila kitengo wataruhusiwa kuendelea na kazi na wawe wamethibitishwa kutoambukizwa. Majina yao yawasilishwe afisini mwangu,” akasema.

Amri sawa na hiyo ilitolewa na Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Utangazaji na Mawasiliano Esther Koimmet ambaye aliwaamuru wafanyakazi wote wafanye kazi kutoka nyumbani.

“Ni wale wanaotoa hudumu muhimu pekee wataruhusiwa kuingia afisini na wadumishe masharti yote ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona,” akasema kwenye taarifa kwa wafanyakazi.

Jumba lote la Teleposta Towers ambako kuna afisi nyingi za serikali litanyunyuziwa dawa ya kuua viini mnamo Jumamosi.

Huduma katika Wizara ya Fedha zimeathirika baada ya wafanyakazi 20 kupatikana na virusi vya corona.

Miongoni mwa huduma zilizoathirika zaidi ni zile za utayarishaji wa pensheni za wafanyakazi wastaafu.

Kwenye taarifa mnamo Julai 15, Katibu katika wizara hiyo Amos Gathecha alisema kuwa wafanyakazi wote katika makao makuu ya wizara hiyo.

“Tumeomba wizara ya Afya iwapime wafanyakazi wote katika afisi kuu za wizara hii, ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya wafanyakazi 200 watapimwa kila siku,” akasema kwenye memo kwa idara zote.

“Kila idara inahimiza kuwasilisha orodha ya watu 40 kila siku ili wapimwe,” Bw Gathecha akasema.

Afisi za PSC jijini Nairobi pia zimefungwa kwa siku 10 baada ya wafanyakazi 10 kupatikana na virusi vya corona. Afisa hizo zilifungwa kwa siku 10, kuanzia Jumatatu, Julai 13.

You can share this post!

KAZI MTAANI: Elungata awaondolea hofu vijana wanaodai wazee...

RIZIKI: Zuio kuingia na kutoka nje ya Nairobi liliathiri...

adminleo