Daktari akaangwa kwa kujisifu kutoa pacha mvulana kwanza ili kuonekana ‘mzee’
NA WANDERI KAMAU
DAKTARI mmoja maarufu amewaacha Wakenya kwenye mshangao, baada ya kusema alimtoa mtoto wa kiume kwanza alipokuwa akimfanyia upasuaji mwanamke ajiyejifungua mapacha, ili aonekane kuwa ‘mzee’ kuliko pacha mwenzake, ambaye ni msichana.
Dkt Mbiti Mondi aliandika ujumbe huo kwenye mtandao wa ‘X’ Jumatatu, Machi 4, 2024 baada ya kumsaidia mwanamke huyo, aliyejifungua mapacha kwa njia ya upasuaji.
Kwenye ujumbe huo, ambao umezua hisia nyingi mitandaoni, Dkt Mwondi alisema kuwa hatua hiyo inatokana na nia yake kumpigania na kumtetea ‘mtoto wa kiume’.
“Dakika chache zilizopita, mwendo wa saa 8.00 usiku, niko kwenye chumba cha upasuaji. Nimetoa mapacha maridadi sana ambao nishawahi kuwaona; mvulana na msichana. Kimakusudi, nilimtoa mtoto mvulana kwanza, ili awe mzee dhidi ya wawili hao. Mtoto wa kiume amuunge mkono mtoto wa kiume. Sikuwa na jingine, ila kumwomba mama yao anikubalie,” akaandika, huku akiambatanisha ujumbe huo na picha ya mapacha hao.
Ujumbe wake ulitajwa kama usiofaa, dakika chache baada ya kuuweka mtandaoni, hasa ikizingatiwa uliandikwa na daktari.
Sababu ni kuwa, alieleza wazi alikiuka kanuni za udaktari, huku akiweka picha ya watoto hao. Pia, alitoa kauli ya kibaguzi dhidi ya mtoto ambaye alimsaidia kumleta duniani.
Maelfu ya watu walioutazama ujumbe huo walimlaumu daktari huyo, kwa makosa aliyokubali kufanya wakati wa upasuaji huo.
Shutuma dhidi yake zilipozidi, aliufuta ujumbe huo.
Ukosoaji dhidi yake ulionekana kutoka karibu sehemu zote duniani.
Dkt Yusuf Mahat kutoka Ireland alisema: “Huwezi kuamua kuhusu mtoto utakayemtoa kwanza. Unamtoa pacha anayejitokeza wa kwanza. Hatua ya kumfikia mvulana kwanza inaweza kusababisha madhara makubwa kwa mama na mtoto.”
Akaongeza: “Hebu tuzingatie na tudumishe kanuni za taaluma yetu. Kuamua mtoto utakayemtoa kwanza si kanuni ya udaktari!”
Akaeleza @Asamoah: “Hawa madaktari wachanga wanahitaji mwongozo. Wana uchangamfu mwingi kiasi kwamba hawajui mipaka iliyopo baina ya maadili na mitandao”.
Kutokana na shinikizo hizo, aliandika ujumbe mwingine, ambapo alionekana kujitetea. Aliwalaumu wanawake kwa “kumwingilia sana”.
“Kinaya ni kwamba, tatizo halitokani na hatua yangu kuweka picha za watoto hao—jambo ambalo mama yao aliniruhusu kufanya hivyo. Naingiliwa kwa sababu nilisema kimzaha kwamba nilimtoa mtoto mvulana kwanza. Ni watu wasioelewa masuala ya kitamaduni,” akasema.
Daktari huyo anahudumu katika Hospitali ya Misheni ya St Damiano, mjini Bungoma.