Habari Mseto

DCI yachunguza kifo cha mtoto katika madrassa Mombasa

Na MISHI GONGO November 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDARA ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) katika Kaunti ya Mombasa inaendeleza upelelezi kuhusu kifo cha msichana mwenye umri wa miaka mitano aliyedaiwa kuanguka kutoka juu ya jengo la madrassa baada ya kufungiwa ndani kama adhabu.

Tukio hilo lililotokea Novemba 18 asubuhi katika Madrassa Tul Nur eneo la Leisure, Nyali, limezua ghadhabu miongoni mwa wakazi na makundi ya kutetea haki za watoto, wanaotaka haki itendeke.

Ripoti za awali za polisi zinaonyesha kuwa mtoto huyo alitenganishwa na wenzake na kufungiwa ndani kama adhabu.

Watoto wengine walipokwenda kucheza, inadaiwa alijaribu kutoroka kupitia dirishani akaanguka na kupoteza maisha papo hapo.

Afisa wa Upelelezi wa Kaunti Ndogo ya Nyali Mohamed Jillo, alisema maafisa wa DCI tayari wameandikisha taarifa kutoka kwa walimu, wanafunzi na uongozi wa madrassa.

“Hili linaonekana kama suala la uzembe. Tunachunguza maelezo yote, kukusanya ushahidi na kubaini iwapo kuna mtu aliyekosa kutimiza wajibu wake,” akasema Bw Jillo katika mahojiano na Taifa Leo afisini mwake.

Aliongeza kuwa, uchunguzi utabaini iwapo madrassa hiyo inafuata kanuni za ulinzi wa watoto zilizo katika sheria ya elimu ya msingi na sheria ya watoto.

Mdokezi kutoka madrassa, ambae hakutaka kutajwa, alisema mama ya msichana huyo alikuwa amemuelekeza mwalimu amuadhibu binti yake kwa sababu alikataa kwenda madrassa asubuhi hiyo. Hivyo mwalimu akamzuia kuungana na wenzake wakati wa mapumziko ya saa nne asubuhi.

Uongozi wa madrassa ulisema hautatoa taarifa kwa sasa hadi uchunguzi utakapokamilika. Kwa upande mwingine, familia ya msichana pia haikutaka kuhojiwa.

Tukio hilo limezua mjadala mkali mitandaoni, watumiaji wakitaka maelezo ya kina kuhusu mazingira yaliyopelekea kifo hicho na kuwataka viongozi wa madrasa kuwajibika.

Mashirika ya kutetea haki za watoto pia yametaka uchunguzi wa kina na kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya wahusika.

Kuhusu madai kwamba wazazi wanashinikizwa kuacha kufuatilia kesi, maafisa wa DCI walisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea kwa uwazi.

Afisa wa watoto mjini Mombasa, Bw Gabriel Kitile, alisisitiza umuhimu wa kutumia mbinu salama kwa watoto katika taasisi zote za elimu, rasmi na za kidini.

“Kilichotokea ni kielelezo kwamba hakuna mtoto anayepaswa kuwekwa hatarini kwa jina la adhabu. Kila kituo cha elimu lazima hakikishe watoto wanawekwa kwa uangalifu na wanalindwa kila wakati,” akasema.

Uchunguzi ukikamilika, faili itawasilishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ili kuamua hatua zinazofaa kuchukuliwa.