DCI yachunguza vifo vya watoto wawili motoni wazazi wakihudhuria ibada kwa jirani
MAAFISA kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) eneo la Suba, Kaunti ya Migori wanachunguza kisa cha moto kilichosababisha vifo vya watoto wawili wazazi wao wakiwa kwenye ibada usiku.
Familia ya watoto hao inadai kuwa mtu au kundi la watu wasiojulikana waliteketeza nyumba yao eneo la Gwassi.
Watoto hao, walifariki wakiwa wamelala ndani ya nyumba moto ulipozuka, wazazi wakihudhuria ibada usiku.
Chifu wa eneo hilo Bw Tobias Opiyo alisema watoto hao walichomeka kiasi cha kutotambuliwa.
“Wazazi ni washirika wa kanisa la Roho. Walikuwa kwenye ibada kwa jirani,” alisema Bw Opiyo.
Bw Opiyo, alisema wazazi hao waliondoka nyumbani saa saba usiku, baadaye walisikia mayowe saa tisa usiku kutoka nyumbani kwao.
Polisi walipeleka miili ya watoto hao katika mochari ya Hospitali ya St. Camillus, Sori, Migori huku uchunguzi ukiendelea.
Imetafsiriwa na Fridah Okachi