• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Del Monte yalilia serikali ya kitaifa iisaidie kutatua mzozo

Del Monte yalilia serikali ya kitaifa iisaidie kutatua mzozo

Na CHARLES WASONGA

WASIMAMIZI na wafanyakazi wa kampuni ya Del Monte Kenya sasa wanaitaka Serikali ya Kitaifa kuingilia kati mzozo kati yake na serikali ya kaunti ya Murang’a kuhusu matumizi ya kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 60,000 ambako kampuni inaendeshea shughuli zake.

Hii ni baada ya majaji watatu wa Mahakama Kuu kukosa kutoa uamuzi kuhusu mzozo kuhusu ukodishaji wa ardhi hiyo wakisema hawana mamlaka ya kuamua suala hilo.

Badala yake, majaji hao – George Kimondo, Wilfred Okwany na Chacha Mwita – waliamuru kesi hiyo inafaa kusikizwa katika Mahakama ya Mazingira na Masuala ya Ardhi.

“Tumevunjwa moyo na uamuzi huu baada ya kesi hiyo kujivuta katika mahakama kuu kwa zaidi ya miaka mitano. Hii ndio maana tunaiomba serikali ya kuitaifa iingilie kati suala hili ili muafaka upatikane kwa manufaa ya wananchi wanaofaidi shughuli za kampuni hii,” Mkurugenzi Mkuu Stergios Gkaliamoutsas aliwaambia wanahabari Jumamosi, Nairobi.

Kiongozi wa wafanyakazi katika kampuni hiyo ni Bw Jacob Mulema.

Wanaiomba Wizara ya Ardhi na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ziongoze mazungumzo kati yao serikali ya Gavana Mwangi Wa Iria ili iongezewe muda wa ukodishaji wa ardhi hiyo. Muda wa sasa wa ukodishaji utakamilika mnamo 2022.

Lakini serikali ya kaunti ya Murang’a imekataa kutoa kibali cha kuiruhusu Del Monte Kenya, inayotayarisha juisi ya mananasi, kuongezewa muda wa ukodishaji ardhi hiyo baada ya 2022.

“Kutotolewa kwa kibali hiki kutaathiri shughuli zetu humu nchini na kupelekea zaidi ya wafanyakazi 6,500 kupoteza ajira. Vilevile, jumla ya wafanyakazi 28,000 wa kampuni zinazowalisha bidhaa na huduma kwa Del Monte wataathirika huku Kenya ikipoteza mapato ya zaidi ya Sh9 bilioni kila mwaka kutokana na mauzo ya bidhaa za nanasi ng’ambo,” akasema Gkaliamoutsas.

  • Tags

You can share this post!

‘Watakaorejesha bunduki wanazomiliki kinyume cha...

Msinisikitikie, Sonko aambia wakazi wa Nairobi

adminleo