Habari Mseto

Deni: Wabunge wageuka maadui wa wananchi

October 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamegeuka maadui wakubwa wa Wakenya kwa kupitisha sheria na maamuzi yanayowaumiza zaidi kwa kuwaongezea gharama ya maisha.

Mnamo Jumatano alasiri wiki hii, wabunge waliipatia serikali kibali cha kuongeza kiwango cha madeni hadi kima cha Sh9 trilioni licha ya wataalamu na mashirika fadhili kuonya kuhusu madhara makubwa kwa uchumi.

Wakati huu Kenya inadaiwa jumla ya Sh5.8 trilioni na mashirika ya kifedha ya kigeni na yale ya humu nchini, kiwango ambacho tayari ni zaidi ya asilimia 50 ya jumla ya utajiri wa nchi, ambao ni Sh11 trilioni.

Katika mwaka huu wa kifedha, bunge lilipitisha bajeti ya kitaifa yenye upungufu wa Sh635 bilioni. Hii ina maana kuwa, pengo hili likizibwa kupitia mikopo, kufikia mwisho wa mwaka huu wa kifedha, madeni ya Kenya yatafikia takriban Sh6.3 trilioni.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Aden Duale na mwenzake wa mrengo wa wachache John Mbadi, wabunge 189 waliokuwa ukumbini wakati huo, waliidhinisha mageuzi katika kanuni kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) na kuipatia serikali idhini ya kukopa hadi Sh9 trilioni. Mageuzi hayo yalipendekezwa na kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani.

“Sharti serikali ipewe nafasi zaidi ya kukopa ili iweze kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo hasa inayolandana na Ajenda Nne Kuu. Hata taifa tajiri kama Japan hukopa kufadhili miradi yake,” akasema Bw Duale.

Naye Bw Mbadi alisema, bila kufafanua, wabunge watahakikisha kuwa serikali inachukua mikopo ya gharama nafuu “ili wananchi wasiumie zaidi”.

Lakini mdadisi wa masuala ya uchumi Paul Masese anasema kiwango hiki cha madeni hakitaiwezesha serikali kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwani sehemu kubwa ya pesa zitakazokusanywa kama ushuru zitatumika kulipia madeni.

“Na hii ina maana serikali italazimika kuongeza aina mbalimbali za kodi, hasa kwa bidhaa za kimsingi, ili iweze kupata peza za kuendeshea shughuli za kimsingi kama kulipa mishahara,” anasema.

Kulingana na Bw Masese, kupungua kwa mapato ya serikali kutachangiwa na changamoto zinazokumba sekta kuu za kiuchumi kama vile kilimo na utengenezaji bidhaa.

“Faida kutokana na mazao kama kahawa, majanichai na miwa imepungua kwa kiasi kikubwa zaidi huku kampuni mbalimbali zikiwafuta wafanyakazi kufuatia kupungua kwa faida. Hii ina maana kiasi cha fedha ambazo serikali hukusanya kama ushuru kinaendelea kupungua,” anasema.

Duru zinasema kuwa wabunge waliipa serikali kuhusa ya kukopa zaidi kwa kupuuza onyo kutoka kwa idara ya masuala ya bajeti bungeni (PBO) kuwaonya kwamba hatua hiyo itaathiri uchumi pakubwa.

“Wakati huu nchi imepitisha uwezo wake wa kumudu madeni. Hii ina maana kuwa nchi haizalishi mapato ya kutosha kuiwezesha kugharamia ulipaji wa madeni. Hatari ni kwamba nchi hii itaendelea kukopa kulipia madeni ya sasa wala sio kufadhili miradi ya maendeleo,” afisi hiyo yenye wataalamu wa masuala ya uchumi na bajeti, ilisema.

Wabunge pia walikwenda kinyume na ushauri wa kamati ya pamoja ya bunge la kitaifa na seneti kuhusu bajeti iliyopendekeza kuwa serikali ipewe ruhusa ya kukopa hadi Sh7.5 bilioni pekee.