Habari Mseto

Dereva ashtakiwa kubandika risiti feki katika chupa 1860 za mvinyo

October 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

DEREVA wa lori la kusafirisha bidhaa alishtakiwa Jumatano kwa kupatikana akisafirisha pombe kwenye chupa zilizokuwa zimebandikwa risiti feki za ushuru.

Risiti hizo zilionyesha kuwa pombe hiyo imelipiwa ushuru, lakini maafisa wa mamlaka ya ushuru nchini KRA walipokagua risiti zilizokuwa zimebandikwa katika chupa 1,860 za mvinyo (pombe) aina ya Sir Antonio Brand Spirit, walibainisha zilikuwa feki.

Bw Paul Wanjohi Mathenge alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi na kukanusha shtaka analodaiwa alilifanya mnamo Julai 19, 2019.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka wa mamlaka ya ushuru KRA Bi Fridah Ombogo kuwa mshtakiwa alikamatwa katika eneo la Litein, Kaunti ya Kericho akisafirisha pombe hiyo na lori nambari ya usajili KBX 592V.

Mahakama ilifahamishwa pombe hiyo ilikuwa imebandikwa risiti feki za ushuru na hivyo kusababisha Serikali kupoteza zaidi ya Sh97,650.

Bi Ombogo alifahamisha korti mshtakiwa alikaidi sheria za ulipaji ushuru zilizopitishwa 2017.

Wakili Michael Osundwa alimweleza hakimu mbali na kutiwa nguvuni, lori alilokuwa analiendesha mshtakiwa lilikamatwa na kufungiwa na maafisa wa mamlaka ya ushuru.

Wakili Michael Osundwa anayemwakilisha Paul Wanjohi. Picha/ Richard Munguti

Aomba dhamana

Bw Osundwa aliomba mahakama imwachilie Mathenge kwa dhamana kisha iamuru arudishiwe lori hilo kwa vile linaendelea kusakama na kuharibika likiendelea kusimamishwa bila kutumika.

Lakini ombi hilo la kuachiliwa kwa lori hilo lilipingwa vikali na Bi Ombogo akisema, “Mshtakiwa anafaa kuwasilisha ombi rasmi ndipo masuala atakayozua yajibiwe na maafisa wa kutekeleza mwongozo wa ulipaji ushuru.”

“Sipingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana lakini nakataa ombi la kuachiliwa kwa lori hadi ombi rasmi liwasilishwe na mshtakiwa kupitia kwa wakili wake Bw Osundwa,” akasema Bi Ombogo.

Akitoa uamuzi Bw Ochoi alimwamuru mshtakiwa awasilishe dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja na akikosa alipe dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu.

Mshtakiwa alilipa dhamana hiyo ya pesa taslimu na kuachiliwa kutoka seli za mahakama ya Milimani.

Pia hakimu alimwamuru mshtakiwa awasilishe ombi rasmi la kutaka lori linalozuiliwa na KRA liachiliwe.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 6, 2019, upande wa mashtaka ueleze iwapo umemkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.